Tarehe Rasmi Ya Kuanza Kwa Uboreshaji Wa Daftari La Kudumu La Wapiga Kura Itatangazwa Baadae
Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (R) Semistocles Kaijage amefungua mkutano wa Asasi
za Kiraia na Tume kuhusu maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura Jijini Dar es Salaam leo na kuwajulisha wadau hao wa Tume kwamba
tarehe rasmi ya kuanza kwa zoezi hilo itatangazwa baadae.
Jaji Kaijage pia
amewajulisha wadau hao kwamba zoezi hilo linalotarajiwa kuanza mwenzi
Julai, mwaka huu (2019) litahusisha "wapiga kura wapya waliotimiza umri wa
miaka 18 na zaidi, au wale watakaotimiza umri huo siku ya Uchaguzi mkuu
ujao".
Ameongeza kuwa
"Kundi lingine litakalohusika katika zoezi hili ni wale watakaoboresha
taarifa zao kama vile, waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika, wanaorekebisha
taarifa zao, bila kusahau wale waliohama kutoka maeneo yao ya awali na kuhamia
maeneo mengine ya Uchaguzi".
Aidha, Jaji Kaijage
amezishukuru Asasi hizo kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiutoa kwa Tume
Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Athumani Kihamia amewaomba wadau wa
Uchaguzi kushiriki kikamilifu katika kuelimisha na kufuatilia zoezi la
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pindi litakapoanza rasmi.
Akizungumza kwenye
mkutano wa Tume na Asasi za Kiraia uliofanyika Jijini Dar es Salaam leo ikiwa
ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari, Dkt. Kihamia amesema ufanisi wa zoezi
la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unategemea ushirikiano wa kutosha
kutoka kwa wadau.
Dkt. Kihamia
amesema lengo la Tume ni kuhakikisha kwamba wale wote wenye sifa wanaandikishwa
kwenye Daftari.
Maafisa wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi kutoka Idara ya Daftari na Tehama wamewaonyesha kwa vitendo
hatua kwa hatua wawakilishi wa Asasi za Kiraia namna ambavyo mpiga kura
anaadikishwa kwa kutumia BVR Kit.
Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (R) Semistocles Kaijage akisalimiana na mwakilishi
wa TEMCO (Tanzania Election Monitoring Committee), Dkt. Benson Bana baada ya
mkutano wa Asasi za Kiraia na Tume kuhusu maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura.
Picha ya pamoja ya
viongozi wa Tume na wawakilishi wa Asasi za Kiraia.
No comments