TAKUKURU Yawasha Moto Waliopiga Bilioni 46 za Libya
Taasisi ya Kuzuia
na kupambana na Rushwa (Takukuru), imetangaza kuwasaka watu wanne wanaodaiwa
kutoweka na zaidi ya Sh bilioni 46, ambazo ni mkopo kutoka Serikali ya Libya
ili kujenga Kiwanda cha Saruji mkoani Lindi.
Akizungumza katika
mkutano na wanahabari jana, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia
Jenerali John Mbungo, alisema fedha hizo kwa Serikali ya Tanzania na Serikali
ya Libya, kama mkopo wenye riba.
Alisema kwa kuwa
Serikali haifanyi biashara, fedha hizo zilikabidhiwa kwa kampuni ya MEIS
Industries Ltd mwaka 2009 kwa ajili ya kujenga kiwanda hicho, lakini hadi sasa
hakijawahi kuonekana na wahusika hawajulikani walipo.
“Mwaka 2009
Serikali hizi mbili zilitia saini mkataba ulioitaja kampuni ya MEIS Industrial
Limited kama kampuni itakayopewa dola milioni ishirini za Marekani kwa ajili ya
uwekezaji wa ujenzi wa kiwanda cha Saruji eneo la Machore mkoani Lindi.
“Fedha hizo
zilitolewa kwa kampuni ya MEIS kama mkopo uliopaswa kurejeshwa kwa riba nafuu
na kwa mujibu wa mkataba, mkopo huo ulipaswa kurejeshwa ndani ya miaka sita,
yaani 2011 hadi 2017. Hata hivyo, hadi mwaka 2019 kampuni hiyo haijarejesha
mkopo huo wala kiwanda cha saruji kilichokusudiwa kujengwa bado hakijajengwa,”
alisema.
Alisema uchunguzi
uliofanywa na Takukuru umebaini kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo imetumika kwa
matumizi mengine kinyume na makusudio ya Serikali jambo ambalo ni kosa.
Brigedia Jenerali
Mbungo alisema wahusika wa kapuni ya MEIS ambao wanatafutwa ni Islam Ally Saleh
Balhabou, Merey Ally Awadh Saleh, Sabri Ameir Kuleib na Abdallah Said Abdallah
bin Aliya, ambao hadi sasa hawajulikani walipo.
Alisema zipo
taarifa kuwa huenda wengine walikimbilia Visiwa vya Comoro na wengine nchini
Uingereza, hivyo juhudi za kuwatafuta zinaendelea.
“Tunatoa wito kwa
yeyote mwenye taarifa sahihi za mahali watuhumiwa hawa wanapoweza kupatikana
wawasiliane nasi ili wakamatwe na kuja kujibu tuhuma hizi zinazowakabili kwa
kuwa kosa hili liko chini ya kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na
kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007,” alisema.
Akitoa ufafanuzi
kuhusu mikopo iliyotolewa na Serikali ya Libya kwa Tanzania, alisema Serikali
ya Libya katika miaka ya 1980 iliikopesha Serikali ya Tanzania mafuta ya petrol
na dizeli kiasi cha tani 200,000 za ujazo ambayo kufikia mwaka 2005 ilikuwa
ikiidai Serikali ya Tanzania Dola 201,000,000.
Alisema kutokana na
fedha hizo, Serikali ya Libya ilisamehe nusu ya deni ambapo Seriali hizo mbili
zilikubaliana namna ya kulipa dola 101,000,000 zilizobaki.
“Katika makubaliano
haya, dola milioni 61 zilitakiwa kulipwa kwa mtindo wa madeni ya kitaifa, dola
milioni 20 zilipwe kwa mpango maalumu na dola 20 milioni zifanye uwekezaji
nchini Tanzania na baadaye zirudishwe Libya kwa riba nafuu,” alisema.
Alieleza katika
mpango huo, kampuni hiyo ya MEIS ilipopewa fedha hizo kwa ajili ya kufanya
uwekezaji nchini ambao ulitakiwa uwe umeshakamilika na urejeshaji wa fedha hizo
nchini Libya kwa riba nafuu uwe umeshakamilika kufikia mwaka 2017.
No comments