Breaking News

WIZARA YA MADINI YAKUSANYA BILIONI 521 NUSU YA KWANZA YA MWAKA WA FEDHA 2024/25

Dodoma - Wizara ya Madini imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 521 katika kipindi cha Julai 1, 2024, hadi Desemba 31, 2024. Hii ni sawa na asilimia 52.2 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1 kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, leo Januari 21, 2025, jijini Dodoma wakati akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji ya Wizara mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Waziri Mavunde amesema mafanikio hayo yanatokana na usimamizi mzuri, udhibiti madhubuti, na weledi katika ukusanyaji wa mapato kwenye sekta ya madini
“Wizara imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na mwaka wa fedha wa 2015/16 ambapo ilikusanya shilingi bilioni 161 kwa mwaka mzima na mwaka huu  ndani ya nusu ya kwanza tayari tumekusanya asilimia 52.2 ya lengo la Shilingi trilioni 1 kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/25”

STAMICO Yapiga Hatua Kubwa

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameongeza kuwa leseni kubwa na za kati za madini ambazo hazijaendelezwa zitarudishwa Serikalini zitakabidhiwa kwa Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) kwa ajili ya kuziendeleza kwa manufaa ya taifa.

Aidha, Mhe. Mavunde amesema kuwa, STAMICO imejipanga kuwa sehemu muhimu ya uzalishaji wa Madini ya Kinywe hapa nchini ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tanzania kuwa kiungo muhimu katika soko la dunia la madini hayo. 
Pia, Waziri Mavunde amefafanua kuwa, katika juhudi za Serikali kuwasaidia wakulima wa chumvi nchini, STAMICO itajenga kiwanda kikubwa cha kusafisha chumvi Mkoani Lindi ili kuimarisha soko la wakulima hao na kwa Mitambo ya kiwanda hicho imeshawasili nchini na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Februari 2025.

Utafiti wa Madini wa Kina Kuimarika

Waziri Mavunde amesema, kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Wizara imegawa nchi katika vitalu sita vya utafiti. Katika mwaka huu wa fedha, asilimia 18 ya nchi itafanyiwa utafiti wa kina ili kuongeza kanzidata ya maeneo yenye madini na kuvutia uwekezaji zaidi.

Pongezi kwa Wizara ya Madini

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Mathayo David, amepongeza juhudi za Wizara ya Madini katika ukusanyaji wa maduhuli na kuimarisha Sekta hiyo.
Vilevile, Mhe. Dkt. Mathayo amepongeza pia uteuzi wa Mhandisi Ramadhani Lwamo kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, akimtaka kutekeleza majukumu yake kwa weledi na bidii ili kudumisha uaminifu wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mnada wa Madini ya Vito Mirerani

Awali, akizungumzia mnada wa madini ya vito uliofanyika Desemba 14, 2024, katika Mji Mdogo wa Mirerani, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini, Augustine Olal, amesema kuwa washindi wa zabuni 47 waliuza madini yenye thamani ya shilingi bilioni 1.13. Serikali ilipata shilingi milioni 80 kama mapato.

Ikiumbukwe kuwa , Wizara ya Madini imepangiwa kukusanya shilingi trilioni 1 katika Mwaka huu wa Fedha 2024/25. Aidha, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaelekeza Sekta ya Madini kuchangia asilimia 10 katika Pato la Taifa kufikia mwaka 2025.

No comments