Manispaa Ya Ilala Yakusanya Sh Bilioni 52…Kuwachukulia Hatua Za Kisheria Wafanyabiashara Wasio Na Leseni Za Biashara,
Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Halmshauri ya
Manispaa ya Ilala imesema kuwa ifikapo Julai Mosi mwaka huu itaanza
kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara wote watakaobainika kufanya
biashara bila ya leseni za biashara.
Aidha, imebainisha
kuwa katika kipindi cha Julai hadi Mei 2018 kukusanya Sh bilioni 52 sawa na
asilimia 92 ya makusanyo hayo huku lengo lilikuwa kukusanya Sh bilioni 56.
Hayo yamesemwa leo
jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Jumanne Shauri wakati
akitoa taarifa kwa wanahabari kuhusu mikakati ya ukusanyaji mapato na
utekelezaji wa miradi.
Alisema kuwa katika
kipindi cha siku 13 manispaa hiyo itafanya oparesheni ya kuwakagua na kuwapa
elimu wafanyabiashara juu ya leseni hizo na kwamba baada siku hizo
kumalizika mkono wa sheria utawagusa watakaobainiki kukaidi kukata
na kulipia leseni zan biashara.
“Kuanzia leo
tunafanya oparesheni na kuwakagua wafanyabaishara na kutoa elimu kama
alivyosema Rais John Pombe Magufuli hatutafunga biashara ya mtu ila watakaoidi
sheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Shauri.
Alisema Kariakoo tu imebainika kuwa na wafanyabiashara wengi wasio na
leseni za biashara ambapo kati ya 13125 ni wafanyabiashara 8671 waliokata
leseni huku akisisitiza Kata ya Jangwani wafanyabiashara 655 pekee walio na
leseni kati ya 955.
Amesisitiza katika
eneo la ushuru wa leseni walitakiwa kukusanya Sh bilioni 8 lakini wamekusanya
Sh bilioni 5 na kwamba ndani ya siku hizo wanalenga kukusanya Sh bilioni 2.8.
Amefafanua kuwa
eneo lingine linalonekana kuwa na makusanyo madogo ni Nyumba za kulala wageni,
ujenzi wa majengo ambapo walijiwekea malengo ya kukusanya Sh bilioni 2 ila hadi
sasa wamepata Sh milioni 400 pamoja na ushuru wa kuzingira majengo makubwa.
Shauri amesema
katika kuhakikisha ndani ya siku hizo wafanyabiashara wanalipia leseni hizo
wanaanngalia uwezekano wa kufanya hadi siku za wikiendi na kwamba malipo hayo
yatafanyikia katika benki zitakazoelekezwa.
Pia amesema
wafanyabiashara watakaokiuka agizo hilo watatakiwa kulipa faini ya kuanzia Sh
100,000 hadi Sh 1000,000.
Bw. Shauri aliongea kuwa halmashauri hiyo tayali imeanza kutekeleza miradi mbalimbali
ikiwemo Ujenzi wa Shule Mpya za Msingi ikiwemo ya Kipunguni Chini na Ulongoni
na Sekondari ya Kinyerezi Annex, Buguruni, na Ukonga Jeshini pamoja na ujenzi
wa madawati ya wanafunzi.
Shauri amesema kuwa
tayari mkataba wa utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa ya
Vingunguti umeshasainiwa na ujenzi unaendelea.
Wakati huo huo,
Mkurugenzi wa manispaa hiyo amesema Juni 24 mwaka huu watatoa Sh bilioni 2 kwa
ajili ya mikopo Wakinamama, vijana na walemavu ambapo gari mbili aina ya
Coaster zitatolewa, Bajaji 50 pamoja na Pikipiki 30.
No comments