RITA Yasajili Bodi Ya Wadhamini Ya Prof Lipumba.
Bodi ya Wadhamini ya Chama Cha Wananchi CUF upande wa mwenyekiti anaetambuliwa na msajili wa vyama vya siasa Prof Ibrahim Lipumba imesajiliwa rasmi na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Naibu katibu mkuu wa CUF Taifa, mhe. Magdalena Sakaya alisema Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imemwandikia barua kuwapa taarifa kuwa maombi yao ya kusajili bodi yamekubaliwa na bodi hiyo imesajiliwa.
"Machi 6 nimepokea Barua kutoka rita ikionyesha kuwa maombi yetu ya kusajili bodi yamekubaliwa na kufahamishwa kuwa imesajiliwa rasmi majina ya wajumbe wote 8 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar yamekubaliwa" Alisema Mhe. Sakaya.
Alisema hatua hiyo imekuja kufatia maamuzi ya mahakama kuu ambayo iliwataka kurekebisha dosari zilizokuwepo awali katika bodi hiyo ili iweze kukidhi vigezo vinavyotakiwa kuwa navyo bodi.
"Mara baada ya kupokea taarifa ya kusajiliwa rasmi kwa bodi kinachofata ni kungoja ikae kikao kuchagua mwenyekiti wake hili kuweza kuanza kutekeleza majukumu yake mara moja" Alisema mhe. Sakaya.
Katika hatua nyingine mhe. Sakaya ametolea ufafanuzi kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama alisema ratiba yake itaendelea kama kawaida kwani hakuna sehemu ambayo inawataka kusitisha shughuli zake za kiutendaji za ndani ya chama.
No comments