Waziri Ummy Mwalimu Atangaza Washindi Wa Shindano La Afya Na Usafi Wa Mazingira ‘Nipo Tayari’
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy
Mwalimu akizungumza na waandishi wa Habari katika mkutano wa tukio hilo Jijini
Dar es Salaam, la kutangaza washindi wa shindano la Afya na usafi wa
Mazingira kwa mwaka 2017, iliyokuwa na kauli mbiu ‘Nipo Tayari’.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akiwa na
nembo ya kampeni ya NIPO TAYARI ambayo inahamasisha usafi wa mazingira hasa
usafi wa kunawa mikono na matumizi sahihi ya vyoo
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh.
Ummy Mwalimu akiwa pamoja na baadhi ya wadau wa Wizara ya Afya katika habari na
nembo hiyo ya NIPO TAYARI.
|
.
Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mapema leo Agosti 11,
2017, imetangaza matokeo ya washindi wa shindano la Afya na usafi wa Mazingira
kwa mwaka 2017, iliyokuwa na kauli mbiu ‘Nipo Tayari’.
Akitangaza washindi hao
mapema leo katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya, Jijini Dar es Salaam Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu amepongeza
wadau mbalimbali kwa kuweza kufanikisha zoezi hilo zikiwemo Halmashauri
zote zilizoshiriki.
“Mashindano ya afya na
usafi wa mazingira kwa mwaka huu 2017 hapa nchini yaliweza kushirikisha
Halmashauri zote zaidi ya 185 huku, Halmashauri 73 zikishindanishwa Kitaifa
baada ya mchujo ngazi ya Mkoa.
Mchanganuo wa
Halmashauri hizi ni; Majiji Manne, Manispaa 21, Miji 21 na Halmashauri za
Wilaya 27.
Kila mwaka, Wizara
yetu imekuwa ikiratibu mashindano haya Kitaifa nchini kote ikiwa na
lengo la kuinua hali ya afya na usafi wa mazingira katika ngazi ya Kaya na
taasisi ili kulinda na kuboresha afya ya jamii.” Amesema Waziri
Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy Mwalimu
amewatangaza washindi wa kwa upande wa Halmashauri za Majiji na Manispaa ambapo
Manispaa ya Moshi ikiibuka kidedea kwa kupata asilimia 78.5, mshindi wa Pili,
Jiji la Arusha, Asilimia 78.1 na mshindi wa tatu, Halmashauri ya Manispaa ya
Iringa, Asilimia 67.2.
Kwa upande Halmashauri
za Miji, mshindi wa kwanza ameibuka Halmashauri ya Mji wa Njombe huku nafasi ya
pili ikichukuliwa na Halmashauri ya Mji wa Kahama na mshindi wa tatu ni
Halmashauri ya Mji wa Tunduma.
Washindi wa Halmashauri
bora inayotekeleza kwa ufanisi Kampeni hiyo hususani katika ujenzi na matumizi
ya vyoo bora, mshindi wa kwanza ni Halmashauri ya Wilaya ya Meru,
kwa mshindi wa Pii imechukuliwa na Wilaya ya Njombe huku wa tatu ni Halmashauri
ya Wilaya ya Makete.
Waziri Ummy Mwalimu
amewatangaza washindi wa Kijiji bora kinachotekeleza kwa ufanisi hiyo ya usafi
ni Kijiji cha Kanikelele kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mshindi wa
pili, Kijiji cha Nambala kutoka Halmashauri ya wilaya ya Meru, na cha tatu ni
Kijiji cha Lyalalo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Aidha Vijiji hivyo
viliweza kupatikana baada ya kushirikisha jumla ya Vijiji na Mitaa 80 huku Kaya
zake zikiwa zimefanikiwa kujenga na kutumia vyoo bora pamoja na sehemu za
kunawia mikono kwa maji na sabuni.
Washindi wengine wa
shindano hilo ni pamoja na Hospitali Bora kwa usafi ambapo Mshindi wa kwanza ni
Arusha Lutheran Medical Centre, mshindi wa pili, Hospitali ya Rufaa ya
Mtakatifu Fransisco na Ifakara – Morogoro na wa tatu, Hospitali ya Rufaa Mount
Meru.
Aidha, Waziri Ummy
Mwalimu amewatangaza washindi kwa upande wa Hoteli, ambapo Hyatt Regency Dar es
Salaam the Kilimanjaro, iliibuka mshindi wa kwanza huku wa pili ikienda
Mount Meru Hotel, Arusha na ya tatu ni Aden Palace Mwanza.
“Wizara itatoa zawadi ya
gari la kubebea taka (trekta lenye tela) kwa Halmashauri ya Mji wa Njombe
ambayo imeibuka mshindi wa kwanza kundi la Miji.
Aidha zawadi ya
gari mpya aina ya Nissan itatolewa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Meru ambayo
ilishika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa
Mazingira, na zawadi za pikipiki aina ya YAMAHA kwa washindi wote waliosalia
ili kutoa motisha kwa mabwana Afya wote.
Pia zawadi nyingine
zitakazotolewa kwa washiriki katika makundi yote ni pamoja Vikombe na Vyeti
maalum ambapo Wizara tutaandaa siku maalum kwa ajili ya kukabidhi zawadi hizo
na tunawapongeza kwa ushindi” alimalizia Waziri Ummy Mwalimu.
Katika kuongeza ufanisi
wa mashindano hayo, Wizara iliunda kamati maalum ambayo iliratibu na kusimamia
zoezi zima la uhakiki wa Mashindano huku wajumbe wakitoka Taasisi mbalimbali
ikiwemo Ofisi ya Rais– TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara
ya Maji na Umwagiliaji, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi – Muhimbili, Chuo Kikuu cha Ardhi,
pamoja na wadau wa Maendeleo wanaojihusisha na shughuli za Afya na usafi wa
Mazingira hapa nchini huku wakizingatia vigezo hali bora ya usafi wa mazingira
kwa ujumla.
No comments