UVCCM WAWABEZA CCM,WADAI MZEE MWINYI HAKUKOSEA KUTOA MAONI YA RAIS MAGUFULI KUONGOZA MILELE
Ndugu Waandishi wa Habari
Kwa heshima kubwa tunawashukuru kwa
dhati na kwa uungwana wenu wa kuitikia wito wetu wa kuwaomba kuhudhuria
mkutano wetu huu ili kuzumgumza nanyi kama ilivyo ada na kawaida na
hatimaye muweze kufikisha ujumbe wetu kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Ndugu Wandishi wa Habari
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni
katika moja ya Baraza la Idd El Fitri lililofanyika katika viwanja vya
Mnazi Mmoja Jijijini Dar es Salam, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili na Mwenyekiti
Mstaafu wa CCM, Mzee Ali Hassan Mwinyi, alitoa maoni yake binafsi baada
ya kuutazama, kuudurusu na kuridhika na utendaji wa Serikali ya Awamu ya
tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli.
Ni ukweli usiofichika wala
kupingika kuwa maoni ya Mzee Mwinyi bila shaka yoyote yatakuwa yamepata
mshawasha baada ya kuvutiwa mno na uchapakazi wa Rais Magufuli, pia maoni hayo
hayakuwa ni uamuzi wala shuruti kama ambavyo baadhi ya watu walivyokishilia
bango na kulishupalia suala hilo kwa mtazamo hasi.
Maoni ya Mzee Mwinyi yalikuwa bayana
au kwa lugha nyingine ni maoni mubashara yanayoweza kumlazimisha kila
binadamu mwenye akili timamu afahamu kwa yakini alichotamka katika
matamshi yake. Alichosema au kushauri ni jambo lenye mantiki
kulingana na mtazamo wake ambao kwa hakika ulijiegemeza chini ya uhalisia
wa mazingira ya nyakati na utendaji wa Rais Dk John Pombe Joseph
Magufuli kwa kadri unavyoonekana.
Kwa bahati mbaya sana, eti wanaojiita
ni wazee wa CHADEMA bila kufanya tafakuri, uchambuzi wa maana katika dhana
kamili yenye uyakinifu wa jambo hilo, jana wakajikuta wakikurupuka, na
kumuandama Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi bila ya kuwa na sababu za msingi
kwa kumtolea maneno yasiyo na kichwa wala miguu.
Tokea Rais Dk John Pombe
Magufuli aingie madarakani baada kuchaguliwa kidemokrasia na wananchi
mwaka 2015, sasa yapata miaka miwili, utendaji wa Serikali yake ya awamu ya
tano licha ya kumvutia kila mtanzania, umeitikisa na kuamsha mjadala nchini,
Afrika Mashariki, Afrika na Dunia nzima .
Mjadala ni kuhusu kipimo cha utendaji
wake unaochukua nafasi pana katika vichwa vya Magazeti ya nje na ndani,
kwenye vipindi vya runinga na mitandao ya kijamii, Kitaifa na Kimataifa
yote ikiwa ni katika kuutazama uadilifu wake, uwazi na uwajibikaji wa
Serikali yake chini ya misingi ya uzalendo.
Watu mbalimbali wamekuwa wakijadili
kutokana na kushawishika kwao Rais Magufuli kuhusu umakini alionao, uchungu kwa
nchi yake na watu anaowaongoza akiwa na azma ya kupigania na kutetea maslahi ya
umma huku akitaka rasilimali za nchi kuinufaisha nchi na watu.
Hakuna mtu au kiongozi wa ndani
au nje ya chama tawala na nje ya nchi waliotumwa wajadili wanavyojadili
iwe kwa kumpongeza na kumsifu kunakofanywa na watu hao.
*Ndugu Waandishi wa Habari*
Waswahili wa kale na wahenga wana
semi mashuhuri isemayo“Kizuri hujiuuza na kibaya Hujitembeza”. Yaonekana ndivyo
inavyotokea kwa walimwengu wanavyoutazama na kuufuatilia uongozi wa Awamu ya
tano chini ya Rais Dk John Magufuli na Serikali yake katika mtazamo chanya wenye
mafanikio.
Alichokisema Mzee Mwinyi si kuwataka
au kuwashawishi wananchi kufanya mabadiliko ya Katiba hatimaye kumpa nafasi ya
vipindi vingine vya utawala Rais John Magufuli abaki madarakani kinyume na
matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Matamshi ya Mzee wetu Ali Hassan
Mwinyi aliyaweka bayana akiyatanguliza utangulizi wa maneno adhimu na
dibaji yaliosema nanukuulaiti nchi yetu isingelikuwa si yenye kufuata
utawala wa kikatiba, Rais Dk John Magufuli alitosha na kufaa kuongoza
nchi yetu kwa siku na miaka mingine.
Umoja wa Vijana ya CCM (UVCCM)
hatuoni kama hilo ni kosa au baa, ama iwe mwao au uonekane uchuro
kutokana na maneno hayo. Mzee Ali Hassan Mwinyi ni mweledi, mlinzi mzuri wa
Demokrasia na mtu anaheshimu Katiba, Katu hakusema na kutaka Katiba ibadilishwe
ili Rais abaki madarakani kama inavyopotoshwa kauli yake.
Ndugu Waandishi wa Habari
Hata hivyo inaonyesha wanaojiita
Wazee wa CHADEMA hawana kumbukumbu ya kutosha. Wamesahau Rais wa
Awamu ya Kwanza Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
alitawala kwa kipindi cha miaka 23 tokea mwaka 1961 hadi mwaka 1985.
Mwalimu Nyerere hakutawala miaka 23
kwa lazima yake, nguvu za udikteta au kutumia misuli ya ubabe, alitawala
kwa matakwa, ridhaa, utashi na maamuzi ya wana nchi wenyewe ndiyo
waliomshinikiza na kumuomba kila wakati abaki madarakani kila alipopania
kujiuzulu na kumpisha mtu mwingine.
Ifahakime kuwa Nchi yoyote na mahali
popote, dunia inahitaji ipate mtawala na utawala wenye tija, manufaa na
maendeleo yanayoonekana, kuwaridhisha au kuwapendezesha na kuwanufaisha
wananchi.
Kushawishika na kuhamasika kwa
wananchi na watu mbali mbali juu ya kazi nzuri inayofanywa na Dkt. Magufuli
nadhani imewakumba mpaka Viongozi wenye nyadhifa mbali mbali katika Vyama Vya Siasa
na makundi mengine. Mfano siku za karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la
wananchi na wanachama wa Chadema wakiwemo madiwani sita kwa hiari na ridhaa yao
wameamua kuachia ngazi na kukikimbia Chadema wakirejea CCM kwa kuridhika,
kutosheka na utendaji wa Serikali ya Rais Dk John Magufuli.
Wanaojiita Wazee wa Chadema
ingelipendeza sana kama wangekuwa na mapenzi na chama hicho wangalikaa chini
kutafakari na kutathmini sababu ipi inayowafanya wanachama, viongozi
waandamizi na madiwani hasa katika Mkoa wa Arusha wakikimbie chama hicho
na kurejea CCM badala ya wazee hao kucheza ngoma isiowahusu.
Ndugu Waandishi wa habari
Wote hapa tunaelewa Katiba ya nchi si
Quran wala Bibilia. Katiba imetungwa kutokana na maoni, weledi na utashi wa
watu. Na watu hao hao kwa kujali kwao mahitaji na matakwa yao,
wanaweza kugeuza chochote ndani ya katiba kwa kujali maslahi yao na wala
isiwe baa au muujiza.
Umoja wa Vijana wa CCM unaamini
ukishafikia hatua ya uzee wakati mwingine unapoteza kumbukumbu muhimu,
tunawakumbusha wanaojiita wazee wa CHADEMA hakuna ushahidi
unaoonyesha Mzee Mwinyi aliwahi kuwa na mpango wa kutaka kujiongezea muda
ili abaki madarakani kama ilivyodaiwa na genge la Wazee hao. Kama mjuavyo kule
Chadema kuna maprofesa wa kuzua hili nalo Mzee Mwinyi wamemzulia na kumpakazia.
Ingalikuwa Mzee Mwinyi alitamani
kujiongezea muda ili aendelee kubaki madarakani kwa wakati ule, angeweza kwa
sababu uongozi wake uliwakuna na kuwapendezesha mno wananchi mijini na vijijini
na wala isingelikuwa ni kazi kubwa ya kukubalika na kuungwa mkono .
Zipo semi na hadithi nyingi zinazodai
Mwalimu Nyerere katika Kitabu chake cha Tanzania na Hatma ya Uongozi
alikiandika kwa lengo la kuwalenga viongozi aliowakusudia kuwapasha na
kutaka wajisahihishe, kujisuta, kujiuzulu au kujirejebisha.
Ukweli ulivyo si hivyo, Mwalimu
kama Mwalimu kitaaluma aliandikia Kitabu chake kwa msukumo wa maono yake
ili kuiasa nchi yetu, viongozi wa sasa na wajao pia kuitazama hatma ya nchi
yetu kiutawala, kidemokrasia na kiutendaji bila kumlenga au kumdhamiria yeyote
kama inavyodaiwa na makuhani wa kuzua.
Ndugu zangu Waandishi wa habari.
Mtu mwerevu siku zote anapotaka
kumuasa mwenzake atoe kibanzi katika jicho lake, kwanza huanza kutoa yeye
boriti katika jicho lake. Kama tujuavyo Katiba za baadhi za vyama vya Siasa
vikiwemo vile vya Ukawa. Katiba zao zinalalamikiwa kwa madai ya kuwa na udikteta.
Tumeshuhudia mivutano
ikirindima ndani ya vyama hivyo huku viongozi wa Vyama hivyo wakigombana
kwa sababu ya kulinda matakwa ya Katiba zao na baadhi yao wamekuwa ni zaidi ya
wafalme na masultani waliojenga himaya ndani ya Vyama vyao huku wakiwa
hawana ndoto wala fikara ya kuachia madaraka.
Wapo wanachama wengine wamefukuzwa na
hata kuvuliwa uanachama ndani ya vyama vya upinzani kwasababu ya kutaka
kuwania nyadhifa za juu ambazo wakubwa hawataki ziguswe kwakuwa kushika nafasi
hizo ni kunagusa maslahi yao.
Wengine wanadaiwa kupoteza maisha
katika mazingira ya kutatatanishi kwa kujaribu kwao kuchukua fomu za kuwania
nafasi za juu huku wagombea urais wengine waliohama toka vyama vingine
walipojiunga na vyama hivyo nyakati za asubuhi, jioni yake wakapitishwa kwa
mbwembwe kuwa wagombea urais kinyume na matakwa ya Katiba zao .
Ndugu Waandishi wa Habari
Mwisho Umoja wa Vijana wa CCM
tunawataka wazee maslahi wa Chadema waache kulishwa maneno na kuwa wazushi na
waongo, waache papara ya kujibu kila wanachokisikia kwa kuchochewa na ushabiki
baada ya kuoayiwa milungula na bahashish na kukimbilia kuwadhalilisha
viongozi waliolitumikia Taifa hili kwa uadilifu na bidii na juhudi huku
wakiongoza nchi kwa hekima, busara kubwa zilizosaidia kuleta
mageuzi kadhaa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yalioacha alama ya
utumishi wao uliotukuka kwa watanzania.
Tunaendelea kuwaaminisha watanzania
Chama Cha Mpainduzi ni chama kikubwa ndani Afrika na duniani kwa ujumla hivyo
siku zote hakifanyi makosa katika kuwaletea viongozi makini, wenye upeo na
uweledi wa hali ya juu.
Ahsanteni
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
No comments