Barrick (Acacia) Wakubali Yaishe.Wiki Ijayo kuanza Mazungumzo na Serikali
Kampuni ya Barrick Gold ya nchini
Canada, imesema wiki ijayo timu ya wataalamu wake watakuja nchini kwa ajili ya
kufanya mazungumzao na Serikali kuhusu uendeshaji wa migodi yake.
Tamko hilo limekuja siku chache baada
ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza kuwa iwapo Barrick inayoimiliki Kampuni ya
Acacia itachelewa kuja kufanya mazungumzo ataifunga migodi yao.
Wakati kampuni hiyo ikijiandaa kuja
nchini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tayari imepeleka madaia ya Dola za
Marekani bilioni 190 ambazo ni sawa na Sh trilioni 424), kwa Kampuni ya Acacia,
ikiwa ni malimbikizo ya kodi kutoka mwaka 2000.
Taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao
wa Financial Post juzi ilisema. “Kampuni ya Barrick Gold kupitia ripoti yake ya
robo mwaka imesema itaanza majadiliano na Serikali ya Tanzania wiki ijayo
kuhusu marufuku ya kusafirisha nje madini na masuala mengine yaliyoikumba
kampuni inayoimiliki ya Acacia.
“Taarifa
hiyo ya mazungumzo inakuja baada ya Jumatatu wiki hii Tanzania kuwasilisha bili
ya dola bilioni 190 kwa Accacia yenye makao makuu Uingereza.
“Serikali
ya Tanzania inaituhumu Acacia, ambayo inamilikiwa na Barrick kwa asilimia 63.9
kudanganya mapato yake ili kukwepa kodi na hivyo kuitaka ilipe malimbikizo
pamoja na faini. Acacia imekana tuhuma hizo.
“Tanzania
pia iliweka marufuku ya kusafirisha mchanga wa dhahabu (makinikia) na fedha
Machi mwaka huu, hatua ambayo inaweza kuathiri asilimia sita ya uzalishaji wa
wakia milioni 5.3 hadi milioni 5.6 ya dhahabu kwa mwaka katika migodi ya
Acacia.
“Barrick ilisema
inasubiri hadi Acacia itakaporekebisha mwongozo wake wa uzalishaji kabla ya
kubadili mwelekeo mzima wa uzalishaji wake kwa mwaka,” ilisema
taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema, Barrick yenye
makao yake makuu Toronto, Canada iliripoti kuongezeka kwa mapato kufikia Dola
bilioni 1.08 robo iliyoishia Juni 30, kutoka dola milioni 138 kwa mwaka mwaka
jana.
“Hilo
lilichochewa na mafanikio makubwa ya mauzo ya hisa katika mgodi wa Veladero na
mradi wa Cerro Casale. Mtiririko wa fedha kwa kipindi hicho ulikuwa dola
milioni 43 ukiwa umeshuka kutoka dola milioni 274 kwa kipindi kama hicho mwaka
jana kutokana na kiwango cha juu cha kodi, ongezeko la mtaji na ongezeko
lililopangwa kwa ajili ya matumizi ya ukuaji wa badaye,” ilisema.
Juni 14 mwaka huu, Rais Magufuli
alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold
Corporation Profesa John Thornton na Ikulu ikatoa taarifa kwa umma kwamba,
katika mazungumzo hayo, kampuni hiyo imesema ipo tayari kufanya
mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza
kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.
Julai 21, 2017 akizungumza kwenye
mkutano wa hadhara mkoani Kigoma, Rais Magufuli alisema. “Nitasimamia haki siku zote katika maisha yangu, na niliwaambia
nimeanzisha vita hii ya kiuchumi, vita ya kiuchumi ni mbaya sana, wakubwa wale
huwa hawafurahi, kuna viongozi wengi tu mliona yaliyowapata ni kwasababu nchi
zao zilikuwa na mali.
“Lakini
wale wakubwa wakataka kuchezea hizo mali, kwa manufaa yao na siyo kwa manufaa
ya wananchi wa pale, walitumia mbinu nyingi za kila aina, lakini Mungu wangu ni
mwema na Watanzania ni wema watasimama kwa ajili ya taifa hili.
“Ninayoongea
nayajua ni matrilioni ya fedha ambayo yameibiwa, na kwasasa hivi tumewaita waje
wafanye mazungumzo, wamekubali lakini wakichelewachelewa nitafunga migodi
yote.
“Ni mara
10 migodi hii tukaigawana Watanzania wachimbe wawe wanauza tuwe tunapata kodi,
kuliko kuchimbwa na watu wanaojiita wawekezaji halafu hawalipo kodi.
“Walikuwa
wanazungumza mle wanachimba dhahabu, madini machache tu, matatu. tumegundua mle
kuna madini mengi.
“Tanzania
hii ni nchi tajiri, lakini imekuwa ikiibiwa mno, tumechezewa sana, mimi nipo
serikalini na mimi ndiye najua siri za serikali, tumechezewa sana kwa kuibiwa
sana mali zetu, kwenye dhahabu huku tumeibiwa mno, ukiyajua yale yaliyokuwa
yanafanyike mle unaweza ukalia.
“Unaweza
ukatamani usiishi, mtu anachimba anapokea anapeleka na anashirikiana na baadhi
ya watu tuliowaamini kwenda kulisimamia hili.
“Anasema
hapa tunasafirisha mchanga na Watanzania wote tunaamini tunasafirisha mchanga,
mbona hawajaja Kibondo kuchukua mchanga wa hapa mbona na penyewe tunao?
“Lakini
tunaamini, wanaupeleka kwenye makontena wanapeleka Ulaya na wakisha enda
kuusafisha kule ule mchanga unaobaki wala hawaurudishi, ulikuwa ni utapeli wa
ajabu, na ni aibu kubwa kuona utapeli huu unafanywa na watu ambao ni wakubwa.
Julai 26 akiwa mkoani Singida, Rais
Magufuli tena alisema “Haiingii
akilini watu wanakuja wanachukua mali zetu na kuondoka nazo, ifike mahali
tuamke, tumeibiwa vya kutosha, nendeni mkachimbe madini, hizo fedha tutagawana
sisi, hata kama hatufanyi kazi hizo fedha tutagawana.
“Wapo
wachina wanakuja kuchimba barabara hapa nchini, tunashindwaje kuwatumia hawa
wakachimbe madini yetu kisha wakatuachia dhahabu yetu halafu wao wakaondoka?
“Mimi
ndiye Rais, hakuna anayejua siri za serikali kama mimi na nawaambia mmepata mtu
ambaye anazungumza ukweli, ningeweza kunyamaza kwa vingine ninavyoviona, lakini
nataka kujenga Tanzania mpya.
“Yale
makontena yote ningeweza kuwaambia tugawane mzee, hata kingereza ninajua,
ningeweza kuwaambia give me ten percent (asilimia 10).
“Ningejenga
mahoteli na kuwa na kampuni nyingi kwani wapo Watanzania wamejenga huko nje
lakini nyumba za wazazi wao zimechakaa, mimi nimezaliwa hapa, ninaishi hapa na
nitakufa hapa,”alisema Rais Magufuli.
No comments