TFRA YAWAVUTIA WAWEKEZAJI SEKTA YA MBOLEA KUTOKA OMAN
Afisa Udhibiti Ubora Mkuu, Esther Kapakala akionesha picha zenye viwango vya virutubisho vilivyomo kwenye mbolea zinazozalishwa na mwekezaji wa kiwanda cha mbolea cha Numo Investment Ndg. Fahad Ali Al Hajri wakati wa mazungumzo ya ana kwa ana baina ya watanzania walioshiriki kongamano na wawekezaji walioonesha nia kuwekeza kwenye tasnia zilizoshiriki, mbolea ikiwepo tarehe 29 Septemba, 2024 nchini Oman.
Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe.Fatma Rajab na washiriki wa Kongamano baina ya Tanzania na Oman wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa leo tarehe 29 Septemba, 2024.
MUSCAT
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ni miongoni mwa taasisi zilizoshiriki katika Kongamano la Kibiashara baina ya Tanzania na Oman lenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uchumi baina ya nchi hizo mbili.
Kongamano hilo lililohusisha takribani watanzania 300 limefanyika leo Septemba 29, 2024 katika Hoteli ya Sheraton iliyopo mji wa Muscut nchini Oman na kuibua wawekezaji katika nyanja mbalimbali ikiwemo tasnia ya mbolea.
Akizungumza katika kongamano hilo mgeni rasmi na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uhamasishaji Uwekezaji wa Oman, Mhe.Qais bin Mohamed Al Yousuf amesema, kumekuwa na ongezeko la asilimia 23.8 la kampuni za kitanzania zilizowekeza nchini Oman kutoka asilimia 13.5 ya kampuni zilizokuwa zimewekeza miaka miwili iliyopita.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe.Fatma Rajab amezungumzia kuendelea kukua kwa ushirikiano baina ya nchi hizo na kueleza nia kubwa ni kuimarisha mashirikiano katika sekta za kilimo na nishati.
Akizungumza na mmoja wa wawekezaji mwenye kiwanda cha kuzalisha mbolea aina ya NPK,Fahad Ali Hajri, Afisa Udhibiti Ubora Mkuu kutoka TFRA, Esther Kapakala ameeleza, vigezo anavyotakiwa kuzingatia ili kufanya biashara ya mbolea nchini kuwa ni pamoja na kusajili kampuni yake kwa kuzingatia vigezo vyote vya kusajili.
Aidha, Kapakala amemshauri mwekezaji huyo kufanya kazi na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kutokana na kampuni hiyo kuwa ni ya Serikali na kumhakikishia ataungwa mkono na shirika ili kufikia hatua njema ya kutimiza nia ya kufanya biashara ya mbolea nchini Tanzania.
Pamoja na hayo, amemwezesha mdau huyo kupata mawasiliano ya kampuni mbalimbali za mbolea ili kufanya mazungumzo nao yatakayomwezesha kuwa na uelewa na uamuzi wa kujihusisha na biashara hiyo nchini Tanzania.
Mwekezaji Fahad Hajri anazalisha mbolea aina za NPK zenye virutubisho vya 12:2:35+TE, 20:20:20+TE na mwisho ni 10:50:10+TE ambapo alielezwa mbolea hizo zitapaswa kusajiliwa kwanza endapo bado hazijasajiliwa nchini.
Akihitimisha mazungumzo baina yao, Kapakala ameeleza kuwa, Mamlaka ina jukumu la kuthibitisha ubora wa mbolea endapo unalingana na ule uliowasilishwa na mwekezaji wakati wa kuomba vibali vya kuingiza bidhaa hiyo nchini ili kuhakikisha wakulima wanapelekewa bidhaa zenye ubora uliodhibitishwa
No comments