Tundu Lissu: Nitanyamaza Nikifa
Mwanasheria Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameachiwa kwa dhamana na
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusema kuwa atanyamaza tu
baada ya kufariki dunia.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida
Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alipata dhamana
jana baada ya mahakama hiyo kubaini hoja za Serikali za kumnyima haki hiyo
hazina mashiko.
Baada ya kutoka mahakamani, alikwenda
katika ofisi za Chadema zilizopo Kinondoni, ambako pamoja na mambo mengine,
alisema ataendelea kuikosoa Serikali hadi pale atakapokufa.
“Hakuna
gereza litakalotunyamazisha, watu wakipelekwa mahabusu watazungumza wakiwa
mahabusu, wakifungwa watazungumza wakiwa kifungoni, hivyo ili wanyamaze itabidi
kwanza wafe… tutanyamaza tukiwa wafu kwa sababu wafu hawasemi,” alisema.
Lissu alisema kuna haki ya kuwasema
na kuwakosoa wale waliopewa madaraka na wananchi.
Alisema katika sheria ya uchochezi ya
mwaka 1953, kutoa kauli yoyote yenye lengo la kukosoa matendo ya Serikali, sera
si kosa na wala kumkosoa rais na Serikali yake si kosa.
“Sasa
ukisema wanakukamata, wanakushtaki kwa uchochezi, wanakupiga, wanakupeleka
central (kituo kikuu cha polisi) au Oysterbay wakikupeleka sio kosa, bali
unatumia akili zako kuikosoa Serikali,”alisema Lissu.
Akizungumzia kuhusu kupimwa mkojo,
Lissu alisema alipelekwa na askari kwenye nyumba iliyo karibu na Ocean Road,
lakini alikataa kutekeleza hilo.
“Niliwaambia
nyie maaskari mimi nimeshtakiwa kwa uchochezi, unathibitishaje uchochezi kwa
kupima mkojo?” alisema Lissu.
Alisema askari hao walimjibu kuwa
kuna vitu wanavitaka, akawaeleza:“Nendeni
mkanishtaki, hamjapata oda ya hakimu, hamtaona mkojo wangu.”
Baada ya kauli hiyo, alisema askari
hao walimwambia kuwa wao wana mamlaka.
“Nikawaambia
mimi ni Rais wa Mawakili (TLS). Siku ukikamatwa, ukaambiwa kupimwa damu, mkojo
waambie hutaki hata kama wamekushtaki.
“Ukitoa
mkojo na usiposaini hakuna dili, walichokuwa wanatafuta wapate dili ya
kutengeneza ‘headline’ (kichwa cha habari), ‘huyu anasema hivi kwa kuwa
anatumia dawa’, nani asiyejua polisi wanabambika? Nikakataa, nikawaambia
mnataka twende kunisachi twendeni.”
Lissu alisema akiwa Segerea alikutana
na wafanyabiashara James Rugemalira na Harbinder Singh Sethi wanaokabiliwa na
kesi ya uhuhumu uchumi na utakatishaji fedha.
“Mwaka
jana nilisema hawa lile dili (kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow) watu lazima
wawajibike, waliowapa hela, waliosaini BoT (Benki Kuu ya Tanzania), walioruhusu
hizo fedha kwa kusema James Rugemalira na Harbinder Singh wapewe wako
wapi?” alihoji.
Lissu alihoji wapi walipo waliopewa
mgawo wa fedha za Escrow.
Kabla ya kutoa uamuzi wa dhamana
jana, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri,
alipitia hoja za pande mbili zilizokuwa zinapingana, zilizowasilishwa
mahakamani hapo mwanzoni mwa wiki.
“Hii kesi
ina dhamana, hoja kwamba anakabiliwa na kesi nyingi zenye viashiria va
uchochezi haina mashiko kwa sababu hakuna taarifa kuwa aliwahi kuruka dhamana.
“Kwangu
mimi hiyo haitoshi kumuweka mahabusu, hoja ya kwamba aendelee kuwepo rumande
kwa usalama wake, hakuna taarifa kwamba akipewa dhamana maisha yake yatakuwa
hatarini.
“Mshtakiwa
anawakilishwa na mawakili 18 wanaomuombea dhamana, wanafanya hivyo kwa upendo
walionao dhidi ya mshtakwa, hivyo haiwezekani akipewa dhamana atadhurika.
“Mahakama
inakubali maombi ya dhamana, mshtakiwa atadhaminiwa kwa masharti ya kuwa na
wadhamini wawili, watasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10 kila mmoja na
mshtakiwa hatakiwi kusafiri bila kibali cha mahakama,” alisema.
Baada ya kutoa masharti ya dhamana,
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi kwa nusu saa ili watafutwe wadhamini hao ambao
walipatikana kwa juhudi za Wakili Peter Kibatala aliyetoka nje ya mahakama
kuwatafuta.
Awali wadhamini hao walishindwa
kuingia eneo la mahakama kutokana na kuimarishwa kwa ulinzi kulikotokana na
kuwapo kwa kesi za ugaidi mahakamani hapo.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali
Mkuu, Simon Wankyo, alidai mahakamani kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika
hivyo aliomba tarehe nyingine ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo
hadi Agosti 24, mwaka huu kwa kuanza usikilizwaji wa awali.
Lissu alidhaminiwa na wadhamini
wawili walioweka dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10 kila mmoja.
No comments