WAZIRI IMBACHAWENE AMTEUA PROFESA WA CHUO KIKUU CHA UDOM KUWA DIWANI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Tamisemi), George Simbachawene amemteua Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM), Profesa Davis Mwamfupe kuwa diwani katika Manispaa ya Dodoma.
Juzi Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma
Godwin Kunambi alimtaja Profesa Mwamfupe pamoja na wenzake wawili Roze Nitwa
(CCM) na Vicent Tibalindwa (Chadema) kuwa waliteuliwa na Waziri kwa mujibu wa
mamlaka aliyonayo.
Kunambi alisema Simbachawene aliteua
majina sita kwa vyama vya Chadema na CCM ndipo wakayapigia kura likiwamo jina
la Mwamfupe aliyetokea CCM.
“Waziri alitumia sheria namba 288
(24) (2d) ya Serikali za mitaa na kanuni za uteuzi za mwaka 2010 sura ya 4 (1)
na 5 (1) vinavyompa mamlaka ya kufanya hivyo bila kuulizwa na humteua mtu
ambaye ni mkazi wa eneo husika,” alisema Kunambi.
Manispaa ya Dodoma haina Meya baada
ya Jaffary Mwanyemba kuondolewa na madiwani Machi mwaka huu kwa madai ya
matumizi mabaya ya madaraka.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alikana
madai ya kumwandaa msomi huo wa uchumi katika nafasi ya Umeya ingawa alisema
kila mtu mwenye sifa za kuwa diwani ana haki ya kugombea nafasi ya uongozi
ikiwamo meya.
Mkurugenzi huyo aliwaondoa hofu
waliokuwa wamejenga nyumba zao katika maeneo ambayo hayajapimwa kabla ya
kuvunjwa kwa CDA akisema hawatasumbuliwa badala yake watarasimishwa huku akitoa
tahadhari kwa wavamizi wa maeneo na viwanja kuwa lazima watavunjiwa.
Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma,
Jumanne Ngede alisema baraza la madiwani halina shaka na uteuzi huo na kwamba
watapewa ushirikiano katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ikiwamo
mchakato wa makao makuu.
Alisema mpango uliopo katika manispaa
hiyo ni kujipanga kuwa na ugeni mkubwa ambao umeingia mkoani hapo ikiwemo
maofisa wa serikali.
Mmoja wa madiwani ambaye hakupenda
kutajwa jina lake alisema mpango wa uteuzi wa msomi huyo unaweza kuwagawa
madiwani kwani kuna kila dalili za kuandaliwa kushika kiti hicho huku wengine
wakitaka apewe nafasi katika kamati ya uchumi na fedha tu ili akaonyeshe uzoefu
wake huko.
No comments