RAIS MAGUFULI HAKUTANA NA MWENYEKITI WA KAMPUNI YA BARICK (ACACIA) IKULU LEO,HAYA NDIO MAKUBALIANO YALIYOFIKIWA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na
Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa
kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L. Thornton na kukubaliana kuwa
kampuni hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa
fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli
zake hapa nchini.
Prof. John L. Thornton ambaye
amesafiri kwa ndege binafsi kutoka nchini Canada hadi Tanzania amekutana na
Mhe. Rais Magufuli leo Juni 14, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam na mazungumzo
yao yamehudhuriwa na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles na Waziri wa
Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.
Baada ya Mazungumzo hayo Prof. John
L. Thornton amesema kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Tanzania yatakayozingatia
maslahi ya pande zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote ambazo inapaswa
kulipa kwa Tanzania.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli
amesema Serikali inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalamu
watakaofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation ili kufikia
makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha
shughuli zake nchini maslahi ya pande zote mbili.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na
kukubali kulipa fedha zinazodaiwa Prof. John L. Thornton amekubali kushirikiana
na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu (smelter) hapa nchini.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli
amevionya vyombo vya habari vinavyowataja Marais wastaafu Mhe. Benjamin William
Mkapa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na kuwahusisha na taarifa za kamati mbili
za uchunguzi wa madini yaliyo katika makontena yenye mchanga wa madini
(Makinikia) ambao ripoti zimekabidhiwa kwake na kamati hizo.
“Nimesoma ripoti zote mbili hakuna
mahali ambapo Mzee Mkapa na Mzee Kikwete wametajwa, vyombo vya habari viache
kuwachafua hawa wazee, wamefanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa letu, viwaache
wapumzike” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Dar es Salaam
14 Juni, 2017
No comments