WAZIRI MKUU ATAKA MKATABA UVUNJWE, MKANDARASI ALIYENYANG’ANYWA PASIPOTI NA RAIS MAGUFULI
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitavumilia wakandarasi wasio na uwezo
na ambao wanapewa kazi lakini wanashindwa kuzimaliza katika muda uliopangwa.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo, jana (Alhamisi, Machi 30, 2017) wakati akizungumza na
watumishi wa Halmamshauri ya Chalinze na wale wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa
Mazingira (CHALIWASA) katika ofisi zao, karibu na daraja la mto Wami, wilayani
Bagamoyo, mkoani Pwani.
Alikuwa
ameenda kukagua mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji Chalinze na ujenzi wa mfumo
wa kusafirisha na kusambaza majisafi pamoja na matenki ya kuhifadhia maji ambao
umechukua muda mrefu lakini haujakamilika. Awamu ya kwanza ilianza mwaka Septemba
mosi 2001 na kukamilika Desemba mosi 2003.
Alimuagiza
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge ahakikishe kuwa kazi ya
ujenzi wa mradi huo inaimarika na kufikia asilimia 80 la sivyo, wakamilishe
taratibu za kukatisha mkataba na kutafuta mkandarasi mwingine.
Agizo
la Waziri Mkuu linafuatia taarifa aliyopewa kwamba mkandarasi wa mradi huo,
Overseas Infrastructure Alliance (OIA) Pvt Ltd ya India alipaswa kumaliza kazi
hiyo Februari 22, mwaka huu lakini hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia
23 tu.
“Nimeelezwa
kwamba mmempatia nyongeza ya siku 100 ambayo inaisha tarehe 31 Mei 2017, kama
kazi yake haitakuwa ya kuridhisha na kufikia walau asilimia 80, itabidi
Mheshimiwa Waziri uendelee na taratibu zako za kukatisha mkataba, tuanze
kutafuta mkandarasi mwingine,” alisema.
“Hii
kampuni niliikuta Lindi kwenye mradi mwingine wa maji kama huu. Nilitoa maagizo
ya kuharakisha ujenzi ukamilike lakini hawakufanya hivyo hadi Mheshimiwa Rais
alipoenda na kuagiza mkandarasi anyang’anywe pasi yake ya kusafiria mpaka
atakapomalizia kazi.”
“Kwa
kifupi ni kwamba hii kampuni haina uwezo wa kufanya hizi kazi, na ndiyo maana
hadi sasa wamekamilisha asilimia 23 tu ya mradi wakati walipaswa kuwa
wamemaliza hivi sasa,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza: “Mheshimiwa Waziri
endelea na utaratibu wa kuwaondoa kisheria sababu hata tukiwaongezea muda bado
hawatakamilisha kazi.”
“Nimesikitika
sana kukuta mkandarasi hajafikia malengo. Mtu akipewa kazi anapaswa awe na
uwezo wa kifedha wa kuifanya ile kazi ili hata Serikali ikichelewesha malipo
yake, yeye aendelee na kazi,” aliongeza Waziri Mkuu.
Akizungumzia
kuhusu ufanisi wa mradi huo, Waziri Mkuu alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa
CHALIWASA, Eng. Christer Mchomba, ahakikishe kuwa wanapeleka maji hadi
majumbani mwa wateja na kuweka mita ili wananchi waweze kulipa bili zao badala
kuishia kutoa huduma hiyo kwenye vioski (viula).
“Kazi
ya kupeleka maji majumbani ni yenu CHALIWASA na siyo ya Wizara. Pelekeni maji
na mfunge mita ili watumiaji waweze kulipa bili zao. Pia toeni elimu kwa
wananchi kupitia mikutano ya hadhara, waelezeni mipango yenu na wapi
mlipofikia. Kazi yenu siyo kutandika mabomba tu, bali kutekeleza majukumu
mliyopewa kwa niaba ya Serikali,” alisema.
Kuhusu
mitambo inayotumika, Waziri Mkuu alisema mashine zilizopo ni za siku nyingi
tangu 2003; hivyo amemuagiza Waziri Lwenge afuatilie upatikanaji wa mashine za
kisasa kwani hilo suala ni kubwa na haliwezi kubebwa na CHALIWASA. “Bora
mngeanza kuagiza mashine mpya hivi sasa, badala ya kusubiri zichakae kabisa,
ndipo muanze kufikiria kuagiza.”
Mapema,
akitoa taarifa ya mradi huo, Eng. Mchomba alisema awamu ya tatu ya ujenzi wa
mradi huo ilisainiwa Mei 18, 2015 kati ya DAWASA na OIA yenye ubia na kampuni
ya Pratibha Industries kutoka India kwa gharama ya dola za Marekani milioni
41.36 ambazo zilikuwa ni fedha za mkopo nafuu kutoka benki ya Exim ya India.
“Kazi
zilizopangwa kufanyika ni upanuzi wa mtambo wa maji ili kuongeza uzalishaji wa
maji kutoka mita za ujazo 500 hadi 900 kwa siku; ujenzi wa mfumo wa mabomba ya
kusambaza maji wenye kilometa 1,022; ujenzi wa matenki makubwa 19 ya kuhifadhia
maji; vituo tisa (9) vya kusukumia maji (booster stations) na vioski (viula)
vya kuchotea maji 351.”
Alisema
hadi sasa mkandarasi huyo amekwishalipwa dola za Marekani milioni 15.81 sawa na
asilimia 38 na anaendelea na ulazaji mabomba ambapo hadi sasa amekwishalaza
mabomba yenye urefu wa km.141 sawa na asilimia 12.4.
Alisema
mradi huo umelenga kuvinufaisha vijiji 68 ambavyo 19 kati ya hivyo viko
Kaskazini mwa mto Wami na 49 viko Kusini mwa mto huo.
Akizungumzia
utendaji kazi wa mkandarasi huyo, Eng. Mchomba alisema Serikali imechukua hatua
za kimkataba dhidi yake kwa kumtoza gharama ya kuchelewa kumaliza mradi
(liquidated damages) kuanzia Februari 23, 2017.
“Pia
mkandarasi amepewa notisi ya siku 100 ya kumtaka aongeze kasi ya kazi,
vinginevyo tutasitisha mkataba ifikapo terehe 31 Mei, 2017 kulingana na
kipengele namba 8.7 cha mkataba,” alisema.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI,
MACHI 30, 2017.
No comments