SWALI LA MHE SALMA KIKWETE KWA WAZIRI MKUU KUHUSU UFISADI WA BILIONI 30 ZA KOROSHO
Mbunge wa Kuteuliwa, Salma Kikwete (CCM), ameeleza kushangazwa
kwa kitendo cha Serikali kukaa kimya juu ya ubadhirifu wa Sh bilioni 30 Bodi ya
Korosho.
Mke huyo wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, alitoa kauli hiyo
bungeni jana wakati akiuliza swali la papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa.
“Umekuwapo ushahidi wa kutosha kabisa
kuhusiana na wizi unaofanyika kwenye biashara ya korosho, hasa katika mikoa ya
Mtwara na Lindi, ukiachilia mbali kazi iliyofanywa na Takukuru iliyobainisha
kwamba kumekuwa na upotevu wa kiasi kikubwa cha fedha shilingi bilioni 30
kutoka Bodi ya Korosho.
“Serikali hatujasikia, mimi binafsi
na wengine hawajasikia juu ya jambo hili. Je, Serikali leo inatuambia nini
kuhusu ubadhirifu huu uliotokea hapa nchini kwetu, hasa wananchi wa Mtwara na
Lindi kwa sababu jambo hili linaweza kutokea sehemu yoyote nchini mwetu,” alihoji.
Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema mienendo ya vyama vya
ushirika nchini imeonyesha si mizuri kwa kuonyesha upotevu wa fedha na
inawakatisha tamaa wakulima.
“Mienendo ya vyama vyetu vya ushirika
nchini vimeonesha si mizuri kwa kuonesha upotevu wa fedha na unakatisha tamaa
wakulima wetu na Serikali inafanya mapitio ya vyama vyote na tumeanza na vyama
vya ushirika wa kilimo.
“Tulikuwa na kikao Bagamoyo kwa ajili
ya ubadhirifu huo wa bilioni 30 na Serikali iliunda timu maalumu na ikagundua
kuwa ni hasara ya Sh bil 6 si bilioni 30 na haikusababishwa na bodi bali vyama
vikuu na vyama vya ushirika vilivyopo kata na wilaya, vyama vya msingi na vyama
vikuu na vyote vilifanyiwa uchunguzi na hatua zimeanza kuchukuliwa,”alisema.
Pamoja na majibu hayo ya Waziri Mkuu, Salma aliuliza swali la
nyongeza akisema haijalishi ni kiasi gani cha fedha kimechukuliwa, lakini
watalipwa lini.
“Haijalishi ni kiasi gani cha fedha
kimechukuliwa, hizi bilioni sita na hizi ni haki za wananchi je, wananchi
wanazipataje fedha hizo?” alihoji
mbunge huyo.
No comments