PROFESA LIPUMBA ATINGA MAHAKAMANI
Mgororo wa ruzuku ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) unazidi
kupamba moto baada ya mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kwenda kuitetea mahakamani.
Profesa Lipumba na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa chama hicho,
Thomas Malima wamefungua maombi Mahakama Kuu wakiomba waunganishwe kwenye kesi
iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa CUF, walio upande wa Katibu Mkuu, Maalim
Seif Sharif Hamad.
Katika kesi ya msingi ya ruzuku namba 21 ya mwaka 2017, wadai
wanaiomba Mahakama imzuie msajili kutoa ruzuku kwa CUF na imuamuru Sh360
milioni alizozitoa kwa kina Profesa Lipumba zirejeshwe kwenye akaunti rasmi ya
chama.
Wadaiwa katika kesi hiyo ni Msajili wa Vyama vya Siasa na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini Profesa Lipumba na Malima wamewasilisha
maombi mahakamani nao waunganishwe kwenye kesi hiyo upande wa wadaiwa.
Maombi hayo yalitajwa jana na Malima aliieleza mahakama wakiwa
viongozi halali wa chama hicho, wanaomba kujumuishwa kwenye shauri hilo kwa
kuwa wana masilahi na shauri hilo.
Wakili wa CUF upande wa Katibu Mkuu, Juma Nassoro na Wakili wa
Serikali, Hang Chang’a waliieleza mahakama kuwa bado hawajapewa hati za maombi
hayo.
Jaji Wilfred Dyansobela aliamuru waombaji hao (kina Lipumba)
kuwapatia nyaraka hizo na amepanga kusikiliza maombi hayo Juni 6, siku ambayo
kesi ya msingi itatajwa.
No comments