MAHAKAMA YATOA AMRI MASOGANGE AKAMATWE
Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu imetoa hati ya kumkamata msanii, Agnes Gerald maarufu kama
Masogange kwa kushindwa kuhudhuria kwenye kesi ya kutumia dawa za kulevya
inayomkabili.
Hati hiyo ilitolewa
jana mbele ya Hakimu Mkazi mkuu, Wilbroad Mashauri, wakati kesi hiyo
ilipotajwa.
Wakili wa Serikali,
Adolf Mkini alidai mahakamani hapo kwamba upelelezi wa kesi hiyo upo hatua za
mwisho, lakini mshtakiwa, wadhamini wake na wakili wake hawakufika hivyo wakili
Nkini akaomba mahakama itoe hati ya kumkamata mshtakiwa huyo kwa sababu ni mara
ya pili ameshindwa kufika mahakamani hapo.
Hakimu Mashauri
alikubali maombi ya wakili wa Serikali na kutoa hati ya kumkamata mshtakiwa
ambaye ni Masogange.
Msanii huyo aliwahi
kuonywa akitakiwa aheshimu mahakama kutokana na kutokuwapo kwenye kesi yake
ilipotajwa.
Katika kesi hiyo
namba 77 ya mwaka 2017, Masogange anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14 mwaka
huu, katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam, alitumia dawa
za kulevya aina ya heroin (Diacety Imophine). Pia inadaiwa kati ya Februari 7
na 14, 2017 alitumia dawa za kulevya aina ya oxazepam.
No comments