DC LINDI AWATAKA WAZAZI KUSHIRIKI KATIKA KUWAWEZESHA VIJANA
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga amewataka wazazi
kuacha tabia ya kuiachia Serikali na mashirika binafsi kuwawezesha vijana na
badala yake washiriki kuwasaidia vijana hao ili waweze kujitegemea.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
nafasi ya Serikali katika kusaidia maendeleo ya vijana waliomaliza mafunzo ya
ufundi chini ya Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na
Shirika la Plan International.
Ndemanga amesema kuwa mradi huo umeleta mabadiliko makubwa kwa
vijana katika eneo hilo kwani wamefundishwa sio tu mafunzo ya ufundi bali pia
ujasiriamali, namna ya kuweka hisa, kujiwekea fedha kwa ajili ya matumizi ya
baadaye pamoja na masuala ya kodi lakini tatizo linalojitokeza ni wazazi
kuwaachia Serikali na wadau wengine kushughulikia kila kitu.
“Changamoto ni nyingi katika kusaidia vijana hasa ambao tayari
walishapata mafunzo kwa sababu wazazi wakishafahamu kuwa vijana wao wako chini
ya mradi basi wanawaachia mzigo wote Serikali na wadau mbali mbali hivyo
nawasihi wazazi wawasaidie vijana wao katika kujitafutia ajira”.alisema
Ndemanga.
Ametoa rai kwa vijana kujitokeza kwa wakati pindi miradi hiyo
inapotokea kwa sababu wengi wao wamekuwa wakichelewesha kuleta maombi hayo
mpaka muda wa mafunzo unafika hivyo kwa kuwa mafunzo hayo hufanyika kwa muda
maalum, vijana wanatakiwa wajitokeze mapema kwa idadi kubwa.
Aidha, Ndemanga amewataka vijana waliopata mafunzo kuwafundisha wenzao
na pia wanaojiajiri wakumbuke kuwaajiri vijana wengine ili kupunguza mrundikano
wa vijana wanaozagaa mitaani bila kuwa na kazi za halali.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Hamida
Mohamed amekabidhi cherehani mbili kwa
vijana wawili waliomaliza mafunzo ya ufundi chini ya mradi huo ikiwa ni njia
mojawapo ya kuhamasisha ushiriki wa wazazi katika kuwakomboa vijana hasa kwenye
masuala ya kiuchumi.
“Mradi huu umetusaidia sana kuwaona vijana wenye mazingira
magumu hasa walemavu na kufahamu matatizo yao hivyo kutufanya sisi viongozi wa
Serikali kufahamu namna ya kuwasaidia huku tukisaidiana na wadau mbalimbali”,
alisema Mhe. Hamida.
Mradi huo wa miaka mitatu 2015 hadi
2018 unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI,
CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan
International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
No comments