PLAN INTERNATIONAL WAZINDUA MPANGO KAZI UTAKAOISAIDIA SERIKALI KUFIKIA SDGs IFIKAPO 2030
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO.
Shirika
la Kimataifa lisilo la Kiserikali la Plan International limezindua Mpango Kazi
wa miaka 5 utakaowawezesha wasichana wanaoishi katika mazingira magumu
kujitambua na kujisimamia wenyewe katika nyanja mbalimbali zitakazowaletea
maendeleo.
Mpango
kazi huo unaanza mwaka 2017- 2022 ukiwa na lengo la kuwasaidia wasichana
1,000,000 ulimwenguni kote.
Hayo
yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kanda ya Nchi za Afrika
Mashariki na Kusini – Plan International, Roland Angerer alipokuwa akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu malengo ya mpango kazi huo.
Angerer
amesema kuwa Shirika hilo limepanga kuisaidia Serikali ya Tanzania kufikia
Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030 kwa sababu mpango huo
umelenga kutengeneza mazingira mazuri kwa watoto hasa wasichana na kuhakikisha
hakuna anayeachwa nyuma katika suala zima la maendeleo.
“Plan
International wameweka mpango mkakati wa ulimwengu mzima ambao utawasaidia
wasichana sio tu katika kupata elimu bali kuwafanya wawe na nguvu itakayowasaidia
kujifunza, kujiongoza, kuamua pamoja na kujipigania katika mambo mbalimbali
yanayowahusu,”alisema Angerer.
Ameongeza
kuwa usawa wa kijinsia ni moja ya Mpango wa Maendeleo Endelevu hivyo wataweka
juhudi kubwa katika kuhakikisha wasichana wanapata haki sawa na wavulana kwani
usawa huo utasaidia kuharakisha maendeleo.
Nae
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo- Tanzania, Jorgen Haldorsen amesema kuwa nchini
Tanzania mpango huo utalenga zaidi katika kuzuia ndoa za utotoni kuanzia katika
ngazi ya Kitaifa hadi Vijiji ili kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki zake.
”Kwa
kushirikiana na Serikali , tumeanzisha miradi ya kuzuia ndoa za utotoni katika
Mikoa ya Mara, Geita,Morogoro na Rukwa na katika mikoa hiyo tunategemea
kuwafikia moja kwa moja wasichana 12,000
na kuwafikia wasichana 120,000 kwa njia zingine tofauti,”alisema
Haldorsen.
Amefafanua
kuwa pamoja na jitihada zote na rasilimali mbalimbali kuelekezwa kwenye jamii
kupitia Mikoa,Wilaya na Kata lakini bado wanatambua umuhimu wa kufanya kazi na
Serikali katika ngazi ya kitaifa kwa kutoa maoni na uzoefu wao katika
kutengeneza sera zinazomuhusu mtoto na usawa wa kijinsia.
Kwa
upande wake Muhamasishaji kutoka Mradi wa Vijana wa ‘Youth for Change’, Upendo
Abisai amelishukuru shirika hilo kwa kufanya jitihada katika kuhakikisha
msichana anapata haki zake kwani ulimwengu mzima wasichana ndio wanaokumbwa na
changamoto nyingi zinazowapelekea kutotimiza malengo yao.
“Sisi
kama vijana wa ‘Youth for Change’ tumepewa fursa kubwa ya kuwafikia na
kuwaelimisha vijana wenzetu juu ya haki zao za msingi pia tuna nafasi ya
kuwasemea wale ambao hawajapata nafasi ya kusema ili kuhakikisha wote kwa
pamoja wanapata haki zao”,alisema Bi. Upendo.
No comments