WAUMINI ANGLIKAN WAMZUIA ASKOFU MOKIWA KUFANYA VIKAO
Askofu
wa Dayosisi ya Dar es Salaam wa Kanisa la Anglikana, Dk valentino Mokiwa jana
alishindwa kuendesha vikao viwili baada ya kundi la waumini kufika Usharika wa
Ilala kwa lengo la kuzuia.
Askofu
Mokiwa, ambaye anapinga uamuzi wa Askofu Mkuu wa Anglikana, Dk Jacob Chimeledya
kumvua madaraka kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, alikuwa aendeshe
vikao vya kamati ya fedha na halmashauri kuu, lakini alilazimika kuviahirisha
baada ya kundi hilo kufika eneo hilo.
Wakati
waumini hao wakizuia vikao hivyo kufanyika, mashemasi, mapadri, wainjilisti na
waumini wa dayosisi hiyo wametoa tamko la kumuunga mkono Dk Mokiwa wakipinga
uamuzi wa mkuu wa kanisa hilo kumvua madaraka.
Askofu
Mokiwa anapinga uamuzi wa kumvua madaraka akisema hauwezi kufanywa na mkuu wa
kanisa, bali na halmashauri kuu ya jimbo ambayo anasema haikushirikishwa zaidi
ya kutaarifiwa uamuzi huo.
Tukio
la jana la kumzuia Dk Mokiwa kufanya mkutano lilitokea saa mbili asubuhi katika
Kanisa la Mtakatifu Nicolau wilayani Ilala, ambako kuna ofisi ya Askofu wa
Dayosisi ya Dar es Salaam.
Mmoja
wa watu walioshiriki kuzuia vikao hivyo, Haule Sylvester ambaye alijitambulisha
kuwa kiongozi wa waumini wa Anglikana jijini Dar es Salaam, alisema walichukua
uamuzi huo kwa kuwa Dk Mokiwa ameshavuliwa uaskofu.
“Huyu
(Dk Mokiwa) hapaswi kufanya shughuli zozote za kanisa kwa sababu si askofu.
Lakini amekuwa akiendesha vikao vya siri na mapadri wanaomuunga mkono,” alisema
Sylvester.
“Jana
(juzi) alifanya kikao cha siri. Leo (jana) alikuwa aongoze vikao viwili,
kikiwamo cha bodi ya fedha ya dayosisi hii, ndiyo maana tumemzuia.”
Alifafanua
kuwa baada ya kikao hicho cha fedha kilichokuwa kimepangwa kuanza saa 3:00
asubuhi, kikao ambacho kingefuata ni cha halmashauri kuu ya dayosisi ambacho
kingefanya uamuzi wa mambo ambayo yangejadiliwa na bodi ya fedha.
Sylvester
alisema kwa mujibu wa katiba ya dayosisi hiyo, vikao hivyo vyote vinatakiwa
viongozwe na mwenyekiti ambaye ni askofu wa dayosisi.
Alisema
halmashauri ina wajumbe 10 akiwamo askofu wa dayosisi, wakati kikao cha bodi ya
fedha kina wajumbe zaidi ya 200 na kina lengo la kupanga bajeti ya mwaka.
“Ki
utaratibu ili kuendesha vikao hivi, lazima uwe askofu wa jimbo la Dar es
Salaam. Tunamsihi Mokiwa aache kufanya kazi na kutumia ofisi kwa kofia ya
uaskofu,” alisema.
Alisema
waumini wengi walipanga kushiriki katika mchakato huo, lakini walienda 20 baada
ya kutoa taarifa polisi.
Alipoulizwa
kuhusu suala hilo, Yohana Sanga ambaye ni ofisa habari wa Dk Mokiwa alisema
vikao hivyo vilikuwa vya kawaida vya dayosisi hiyo na vililenga kujadili
maendeleo ya kanisa.
“Tulishangaa
kuona kundi lile la watu, ambalo chimbuko lake limetoka Kanisa la Magomeni
linalompinga Askofu Mokiwa,” alisema.
Mbali
na kundi hilo, kilichowasikitisha zaidi ni kuona magari sita ya polisi,
wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), yaliyokuwa yameegeshwa nje ya
kanisa.
Hata
hivyo, Kamanda wa Polisi wa Ilala, Salum Hamduni alisema kuwa askari hao walikuwa katika doria ya
kawaida.
Sanga
alisema baada ya kundi hilo kufika katika eneo hilo, liliingia moja kwa moja
kanisani na walipowauliza walijibiwa kuwa wanakwenda kujadili masuala ya
kanisa.
Alisema
baada ya kuona hivyo, walisita kufungua ofisi iliyoandaliwa kwa ajili ya vikao
na baada ya majadiliano ya muda mrefu, waliahirisha.
“Walivyoona
hatufungui ofisi, waliamua kuondoka kwa mafungu.Lengo lao lilikuwa kuvunja
vikao hivi,” alisema Sanga.
Taarifa
ya viongozi hao wanaomuunga mkono Askofu Mokiwa, inasema bado wanaendelea
kumtambua na kumuunga mkono kiongozi huyo kama askofu wa Dayosisi ya Dar es
Salaam na kwamba uamuzi uliochukuliwa dhidi yake ni batili.
Hivi
karibuni, Askofu Mkuu, Chimeledya alimtaka Dk Mokiwa ajiuzulu kwa kile
alichodai kuwa anatumia vibaya madaraka yake na ubadhirifu wa fedha.
Hata
hivyo, Dk Mokiwa alikanusha madai hayo na kusema mgogoro wa kanisa hilo ni wa
kutengenezwa na maadui zake.
No comments