JECHA AIBUKA NA KUTAJA SABABU ZILIZOPELEKEA KUFUTA ZANZIBAR.
Baada ya kimya kirefu, hatimaye Mwenyekiti wa Tume
ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha amefunguka na kuelezea kuwa
uamuzi aliouchukua wa kufuta uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2015 baada ya
kubainika kuwa na dosari, ulifanyika kwa kufuata taratibu, kanuni, Sheria na
Katiba ya Zanzibar.
Jecha
aliyasema hayo wakati akihojiwa na kipindi cha Funguka, kinachorushwa na Kituo
cha Televisheni ya Azam na kusisitiza kuwa, hana wasiwasi wala hofu yoyote kwa
hatua hiyo, aliyoichukua ya kufuta uchaguzi kwa kuwa ilifuata misingi yote ya
Sheria na Katiba.
Pamoja
na kwamba alikataa kujibu kwa undani kuhusu hatua yake hiyo na kusisitiza kuwa
mengi atayabainisha kwenye taarifa ya tume, alisisitiza kuwa hakuwahi kutumika
na chama chochote wala kuwasiliana na Rais Ali Mohammed Shein kama
inavyodhaniwa na wengi.
“Haya
yote yataonekana kwenye taarifa ya uchaguzi, siwezi kuongea hapa sasa ila
kiukweli utaratibu ulifuatwa. Matokeo yalifutwa kutokana na dosari
zilizojitokeza ikiwemo baadhi ya matokeo kujulikana kabla na kusababisha baadhi
ya vyama kulalamika,” alisisitiza Jecha.
Alieleza
kuwa matatizo na dosari za uchaguzi huo, yalianza kujitokea katika kipindi cha
kupokea matokeo ambapo matokeo yalitoka katika maeneo ya Unguja, hayakubainika
kuwa na matatizo, isipokuwa kwa matokeo yalitoka katika maeneo ya Pemba.
Alisema
katika kura hizo za Pemba, ilibainika kuwa utaratibu wa kiufundi ulifanyika
kuharibu matokeo ya hesabu za kura baada ya kufanyika urekebishaji wa kasoro wa
mambo, ambayo hayakutakiwa yafanywe nje ya sheria za uchaguzi.
Alisema
baada ya kutokea kwa dosari hizo, kwa upande wa tume kupitia yeye, iliamua
kufuta uchaguzi mzima ili kuepusha vurugu na mgongano wa kisiasa huku Polisi
ikifanya uchunguzi kuwabaini wahusika waliosababisha dosari hizo katika matokeo
ya uchaguzi.
Kuhusu
kushirikisha wajumbe wengine wa tume katika kufanya maamuzi ya kuufuta
uchaguzi, Jecha alibainisha kuwa tume nzima ya ZEC ilihusika katika kufutwa kwa
uchaguzi huo na ndio maana baada ya kufutwa taratibu za uchaguzi mwingine
zilitekelezwa vyema na tume hiyo.
Hata
hivyo, alibainisha kuwa katika kutangaza uamuzi wa kufuta uchaguzi huo,
alilazimika kufanya hivyo binafsi baada ya kuona hali ya matokeo hayo inazidi
kuwa mbaya na kwenda kinyume cha taratibu za uchaguzi.
Alibainisha
kuwa baada ya kufuta uchaguzi huo, ili kuleta usawa kwa vyama vyote, tume hiyo
ilisubiria vikao vya kutafuta mustakabali wa kisiasa visiwani humo vilivyokuwa
vikifanyika baina ya viongozi wa kisiasa wa vyama vyote ndipo itangaze tarehe
ya uchaguzi mpya.
“Tulikaa
kimya kwa takribani mwezi mmoja tukisubiri hatua zichukuliwe na viongozi
kupitia hivyo vikao vyao. Tulisubiri katika ule muda bila kuvunja sheria, na
baada ya kuona hakuna hatua zinachokuliwa dhidi ya maamuzi yetu tulitangaza
tarehe ya uchaguzi,” alieleza Jecha.
Mwenyekiti
huyo alikanusha madai kuwa ametumika kufuta uchaguzi huo kwa maslahi ya CCM na
Dk Shein. “Hapana, Sijawahi hata mara moja kuitwa au kutafutwa na kiongozi
yeyote wa serikali, wala Rais sijawahi kuwasiliana na hata namba yake sina,”
alifafanua.
Alisema
ingawa hajawahi kukutana na mtu yeyote anayemlaumu kuhusu uamuzi wa tume hiyo
wa kufuta uchaguzi, endapo kuna mtu bado ana malalamiko, anaruhusiwa kuiandikia
ZEC malalamiko yake na si yeye binafsi, yatafanyiwa kazi.
Pamoja
na hayo, mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa hata baada ya kuufuta uchaguzi huo,
kwa kuwa anaamini alifuata taratibu na sheria zote, hakujificha wala kuogopa
kitu, kwani aliendelea na shughuli zake kama kawaida.
“Hadithi
zilikuwa nyingi, kila mmoja alifikiri alivyotaka yeye, mie nilikuwepo Zanzibar
natembea, lakini si kila mtu alikuwa ananiona. Redio za kijamii kila moja
ilikuwa inazungumza vyake, mwenyekiti yuko hivi, mwenyekiti yuko wapi,
mwenyekiti kesho ananyongwa mara nimepelekwa mahakama za kimataifa yote hayo
yalizungumzwa lakini mie nipo,” alisema.
No comments