MIKATABA 9 ILIYOSAINIWA NA SERIKALI YA TANZANIA NA UTURUKI LEO
Serikali
ya Tanzania na Serikali ya Uturuki zimesaini mikataba tisa ya makubaliano ya
kiuchumi inayolenga katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa maendeleo
baina ya nchi hizo.
Mikataba
hiyo inahusisha sekta za uchukuzi, mawasiliano, habari, elimu, utalii, utafiti,
viwanda, afya na ulinzi.
Akizungumza
mara baada ya kusaini kwa mikataba hiyo
leo Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. John Magufuli alisema ujio wa Rais wa Uturuki na ujumbe wake ni kielelezo
cha ukuaji wa mahusiano baina ya Tanzania na Uturuki katika nyanja ya biashara
na kimaendeleo baina nchini hizo.
Rais
Magufuli alisema katika mazungumzo yake aliyofanya na Rais Recep Erdogan kuhusu
ujenzi wa Reli ya Standard Gauge nchini, alimjulisha kiongozi huyo kuwa
miongoni mwa wakandarasi walioomba zabuni ya ujenzi wa reli hiyo kuwa ni
kampuni kutoka Uturuki, hivyo endapo itashinda zabuni hiyo itasaidia kukuza
uhusiano uliopo baina ya nchi hizi mbili.
Aidha,
Rais Magufuli alisema kuwa, Serikali ya Tanzania inatarajia kuomba mkopo kupitia Benki ya Exim ya Uturuki katika
kujenga sehemu ya kipande cha ujenzi wa reli hiyo.
Rais
magufuli alisema Tanzania inaendelea kunufaika na uwepo wa Shirika la Ndege la
Uturuki kwa kufanya safari zake za moja wka moja kutoka nchini Uturuki, kwa
kuwa utasaidia kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini na hivyo kukuza uchumi wa
nchi hizo.
Kwa
upande wake Rais wa Uturuki, Recep Erdogan alisema kuwa uwepo wa mikataba hiyo
baina ya Tanzania na Uturuki itasaidia kupata matokeo mazuri ya uhusiano pamoja
na fursa mbalimbali za ushirikiano katika nyanja ya Kilimo, Utalii, Ulinzi,
Reli ambazo zitawezesha kukuza uchumi wa mataifa hayo.
Rais
Erdogan alisema kuwa Uturuki imelenga kukuza ushirikiano uliopo baina yake
na Tanzania kupitia makongamano ya
wafanyabiashara yenye malengo ya kukuza uchumi, kuongeza ajira pamoja na kukuza
ujasiriamali baina ya Tanzania na Uturuki.
“Kiwango
cha Biashara ya uwekezaji katika nchi ya Uturuki ni Dola za kimarekani 150
ambapo lengo letu ni kufika Dola za kimarekani 500,” alisema Rais huyo.
Aidha
Rais Erdogan alisisitiza kuwa kufanya kazi kwa pamoja kutasaidia nchi hizi
kusonga mbele na kufanikiwa katika nyanja mbalimbali.
Nae
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe alisema kuwa makubaliano
ya mkataba baina ya Tanzania na Uturuki katika Sekta ya Utalii yatasaidia
katika kutangaza vivutio vilivyopo nchini, kubadilishana wataalamu,
kubadilishana taarifa na kuongeza idadi ya watalii nchini.
Prof.
Magembe aliongeza kuwa makubaliano hayo yatakuza sekta ya utalii katika kuvutia
uwekezaji wa katika maeneo ya hoteli, fukwe na mbuga za wanyama zilizopo
nchini.
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
No comments