Breaking News

CCM YAELEZA SIRI YA USHINDI, YATOA NENO KWA WAPINZANI 2020


Ikiwa zimepita siku mbili baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuibuka na ushindi wa Kata 19 kati ya 20 na Jimbo la Dimani, katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Januari 22, 2017.

Kimeeleza siri za ushindi huo, huku utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya tano chini Rais John Magufuli ukitajwa kuwa kivutio cha wananchi wengi kupigia kura wagombea wa CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole amesema siri nyingine ya ushindi huo ni utekelezwaji wa ahadi zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ikiwa ni pamoja na ahadi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, vita dhidi ya ufisadi, rushwa na ubadhirifu wa mali za umma pamoja na ununuzi wa ndege mbili za shirika la ndege ambazo zinachangia ukuaji uchumi wa nchi na sekta ya utalii.

"Vita dhidi ya ufisadi na rushwa inayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano, utekelezwaji wa ahadi zilizoahidiwa katika kipindi cha kampeni za uchaguzi 2015, ndio siri kuu mbili za ushindi wa CCM," amesema.

Pia Polepole amejibu tuhuma za Chama cha Wananchi (CUF)dhidi ya CCM ambapo iliituhumu CCM kuwa imeshiriki kuvuruga uchaguzi na kuiba kura  na kwamba ndio chanzo cha Mgombea wake katika jimbo la Dimani, Abdulrazak Ramadhani kushindwa.

Polepole amekana tuhuma hizo na kuitaka CUF kujitafakari ilipoanguka badala ya kulaumu chama chake.

Matokeo ya Dimani yamedhihirisha CUF ilikua tatizo tangu uchaguzi uliopita, 2015 CCM ilipata kura 4400,  CUF 2300, 2017 CCM imepata kura 4860 sawa na asilimia 78, CUF wamepata 1200 anguko la zaidi ya 50%. CUF wamtafute mchawi juu ya kushindwa na anguko lake yuko ndani ya chama chao hasa Zanzibar," amesema.

Aidha, Polepole ametuma salamu kwa vyama vya upinzani juu ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020, ambapo amesema chama chake kiko katika hatua ya kujiimarisha pamoja na kufanya  uchaguzi wa viongozi.


"Baadhi ya wanasiasa wanatutisha kwamba 2020 tutakutana na tutaachia madaraka, kama wanatutabiria giza, kwetu CCM tuna mwanga mkubwa unaotupa hamasa ya kuwatumikia watanzania kwa moyo, uadilifu, umoja ili kuwaletea maendeleo ya haraka," amesema

No comments