ALIYETOBOLEWA MACHO AKUTANA USO KWA USO NA MTOBOA MACHO 'SCORPION'
Kwa
mara ya kwanza mshitakiwa katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na
kujeruhi, Salum Njwete maarufu Scorpion, amekutana na mlalamikaji katika kesi
hiyo, Said Mrisho katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, iliposikilizwa jana.
Mrisho,
ambaye ndiye shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, aliieleza mahakama hiyo kuwa
alichomwa visu tumboni na mgongoni kabla ya kutobolewa macho.
Akiongozwa
na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule,
Mrisho alidai kuwa wakati tukio hilo linaendelea, alimkariri mshitakiwa kwa
kumuangalia usoni.
Akielezea
tukio lilivyotokea, alidai Septemba 6, mwaka huu saa nne usiku alikuwa kazini
kwake Tabata Segerea kwa kazi yake ya kinyozi na baada ya kufunga ofisi,
alikwenda kituoni kusubiri usafiri wa kwenda nyumbani kwake Makuburi, karibu na
Ubungo.
Alidai
wakati anasubiri usafiri, ilipita bajaji na kumuuliza anakokwenda, ambapo
alimwambia kwamba anakwenda Ubungo na mwenye bajaji alidai anakwenda Buguruni,
ila anaweza kumsogeza hadi Tabata Relini ili akapande magari ya Ubungo.
‘’Wakati
nishapanda bajaji na tumeelewana anifikishe Tabata Relini ghafla dereva huyo
aliniomba apite njia ambayo ni fupi kutokezea Buguruni, ambapo hapo ndiko
nitakapochukulia magari ya Ubungo kwani naishi Makuburi,” alidai Mrisho.
Alidai
baada ya kufikishwa Buguruni Kwa Mnyamani, aliona wauza kuku na kusogea kwa
ajili ya kununua ili kupeleka nyumbani kwake.
‘’Kulikuwa
kuna wafanyabiashara wengi wa kuku eneo la Buguruni kituo kinaitwa Kwa Mnyamani
kama saa 4:40 usiku ambapo nilinunua kuku mmoja kwa Sh 6, 000,” alidai.
Akiendelea
kutoa ushahidi, Mrisho alidai wakati anaendelea na manunuzi na kuongea na
muuzaji, aliona mtu amesimama upande wake wa kulia na alianza kumuita.
‘’
Aliniambia ‘broo’ nina shida. Nami nilimgeukia na kumuuliza una shida gani kama
una shida sema nakusikiliza kama naweza kukusaidia nikusaidie, lakini mtu huyo
hakujibu ambapo niliendelea na manunuzi,’’alidai.
Shahidi
alidai wakati anaendelea na manunuzi alishikwa na hofu, kwani mkono wake
alikuwa amevaa cheni ya silva na mfuko wa suruali, ulikuwa na fedha iliyokuwa
inaonesha kutuna.
‘’Ghafla
nilishtukia ninachomwa visu mkononi na bega la kushoto ambapo nilipogeuka
niliendelea kuchomwa na nikaanza kupiga kelele ya mwizi lakini sikupata msaada,
kwani nilishangazwa kuona watu wananiona lakini hawanipi msaada,’’alidai na
kuongeza:
‘’Yule
mtu alijibu hakuna mtu wa kumsaidia ambapo aliendelea kumchoma visu vinne tumboni
na kuanguka chini wakati huo kuna watu walikuwa wanamwita Scorpion, kwamba
tayari umeshaua huku akiendelea kunikagua mfukoni,’’alidai.
Alidai
wakati anaendelea kukaguliwa, mshitakiwa alimkanyaga mkono wake na kumkata
cheni ambayo alikuwa amevaa mkononi na shingoni. Pia, alidai kuwa alivyodondoka
chini alidondoka chali kwa hiyo alikuwa na nafasi ya kumkariri vizuri jinsi
alivyo, kwa kuwa kulikuwa na mwanga wa taa.
Aliiambia
mahakama kuwa, mshitakiwa aliendelea kumkagua mfukoni na kuchukua fedha zote na
kwamba alisikia sauti kuwa, “Salum mwache huyo keshakufa sasa ukimchukulia na
simu ndugu zake watajulishwaje?” Shahidi alidai baadaye alivuliwa fulana na
kumfunga mkononi kisha akamburuza kumpeleka barabarani huku akiwaambia wenye
magari wamgonge.
“Muda
huo nilikuwa sijatobolewa macho ambapo niliwekwa barabarani ili nigongwe na
gari, lakini yalikuwa yananipita nilikaa barabarani kama nusu saa wakati huo
yeye kasimama pembeni. “Baada ya muda alinivuta pembeni na kunipiga kisu cha
jicho la kushoto ambapo nilipoteza fahamu kwa muda na baadaye nilisikia mtu
anadai yeye ni raia mwema anataka kunisaidia ambapo nilimpa simu na kuanza
kuwasiliana na ndugu zangu,’’alidai.
Shahidi
huyo alidai baada ya muda alisikia gari la polisi limefika na kumchukua hadi kituoni
kwa ajili ya kupewa Fomu Namba Tatu(PF3) kwa ajili ya matibabu.
Aidha,
alidai kwa kuwa alikuwa anasikia maumivu, alichukuliwa maelezo akiwa ndani ya
gari ambapo baadaye alifikishwa Hospitali ya Amana na kupewa huduma ya kwanza.
Shahidi
huyo alidai alipofika Amana, alikutana na ndugu zake na baada ya muda
alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo alipewa kitabu cha kusaini kwa
ajili ya kufanyiwa upasuaji tumboni.
Pia
alidai baada ya muda, daktari wa macho alimfanyia uchunguzi na kueleza kuwa
macho yametobolewa, ambapo alikaa hospitali kwa siku sita.
Kabla
ya kuanza kutoa ushahidi huo, mshitakiwa ambaye alipandishwa kizimbani saa 3.35
asubuhi, aliomba mahakama isianze kusikiliza shauri hilo hadi wakili wake wa
utetezi afike.
Mahakama
hiyo ilikubaliana na ombi hilo, ambapo baada ya dakika 15 kupita wakili alifika
na kuanza na usikilizwaji.
Kwa
mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa ambaye ni mwalimu wa karate, alitenda
kosa hilo Septemba 6, mwaka huu maeneo ya Buguruni Sheli wilayani Ilala.
Ilidaiwa
mshitakiwa aliiba cheni ya dhahabu gramu 38 yenye thamani Sh 60,000, kibangili
cha mkononi na Sh 331,000 pamoja na pochi, vyote vina thamani ya Sh 476,000,
mali ya Said Mrisho.
No comments