WAFUASI WA CUF WACHAPANA MAKONDE MAHAKAMANI DAR
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana
iligeuka kuwa uwanja wa masumbwi, baada ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF)
kupigana na kusababisha watu watatu kujeruhiwa.
Wafuasi hao ni wa Bodi ya Wadhamini ya Chama
walio upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na wanaomuunga mkono
Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea kabla ya
kuingia kwenye chumba cha mahakama, tayari kwa kusikiliza uamuzi wa kujitoa au
kuendelea kwa Jaji Sekiet Kihiyo kusikiliza kesi hiyo na baada ya kutoka
mahakamani.
Hata hivyo, Jaji Kihiyo alitupilia mbali maombi
ya bodi ya wadhamini kwamba asiendelee na kesi hiyo, kwa madai kwamba hawana
imani naye, kwa kusema kuwa maombi hayo, hayana msingi kwa kuwa sheria
inamruhusu kutojitoa kirahisi kwenye kesi.
Alieleza kuwa wadau hawana nafasi kujichagulia
jaji wanayemtaka. Kabla ya kuingia kwenye chumba cha mahakama, mfuasi mmoja wa
Profesa Lipumba na wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Maalim Seif, walianza kurushiana
ngumi na kuleta mtafaruku katika eneo la watu wanaosubiria kesi zao kuitwa huku
Lipumba akionekana kulindwa na walinzi mbalimbali.
Aidha, baada ya jaji kutoa uamuzi huo, wafuasi
wote walitoka nje, ambapo wakati Profesa Lipumba akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu kesi hiyo, wafuasi hao walianza kupigana na kujeruhi watu watatu,
ambapo mmoja wao, aliyejulikana kwa jina la Robert Samson, alijeruhiwa kwa
kutumia kitu chenye ncha kali shingoni na kusababisha kuvuja damu nyingi.
Hali hiyo iliendelea kwa wafuasi wa bodi ya
udhamini, kulalamikia walinzi wa mahakama, kwamba ni kwa nini wanakagua watu,
lakini wameshindwa kuwaona wenye silaha, ikiwemo visu na kusababisha watu wao
kujeruhiwa.
Pia walidai kuwa licha ya kuwepo kwa askari
wengi mahakamani hapo wakiwa na silaha, walishindwa kutuliza ghasia hiyo,
ambayo imeleta madhara, kwa kuwa kila mfuasi aliyemuona adui yake alishikana
naye shati na kupigana.
Kabla ya vurugu hizo kuisha, Profesa Lipumba na
wafuasi wake walipanda magari yao huku wakimwimbia nyimbo za kumsifu mwenyekiti
huyo na kuondoka. Waliwaacha wafuasi wa bodi ya wadhamini, wakilalamikia
kitendo cha kupigwa.
Walijiapiza kwamba watajipanga ili siku kesi
hiyo itakapoitwa tena, watahakikisha wanawadhibiti wapinzani wao na kwamba
wataleta madhara makubwa mahakamani hapo.
Awali, akitoa uamuzi huo, Jaji Kihiyo alisema
kuwa Novemba 10 mwaka huu, mawakili wa bodi ya wadhamini ya CUF, wakiwakilishwa
na Rahim Khalfan, waliandika barua kwa Msajili wa mahakama hiyo, kuomba jaji
huyo ajitoe, kwa kuwa wateja wao hawana imani naye.
Alisema kuwa hawezi kujitoa, kwa sababu zisizo
za msingi, kwamba anaupa upendeleo upande wa washitakiwa na kuwaacha waombaji
wakati hakukuwa na mazingira ya kuruhusu kutolewa hoja kwa pande zote.
“Mahakama ya Rufaa inasema majaji au mahakimu
hawatakiwi kujitoa kwa urahisi kwenye kesi. Pia sheria hairuhusu wadau ambao
wanakuja kwa mara ya kwanza mahakamani na hawajui taratibu za mahakama watake
kujichagulia jaji,” alisema Jaji Kihiyo.
Alisisitiza kuwa jaji au hakimu ana mamlaka
chini ya sheria, kujitoa au kuendelea kusikiliza shauri, kama ataridhika kwamba
sababu zilizotolewa, zina nguvu ya kushawishi afanye hivyo.
Chanzo-Habarileo
No comments