WAZIRI NAPE, KUTOA LAKI TANO KWA KILA GOLI LA SERENGETI BOYS
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Moses
Nnauye akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo Pichani) kuhusu mchezo kati
ya Serengeti Boys na Congo-Brazaville utakaofanyika Septemba 18 katika Uwanja
wa Taifa Jijini Dar es Salaam. Picha na May Simba WHUSM
Na Lorietha Laurence-WHUSM.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na
Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye ameahidi kutoa shilingi laki tano kwa
kila goli litakalofungwa na timu ya Serengeti Boys katika mchezo wa
kuwania kufuzu fainali za Kombe la mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri
wa miaka 17 utakaofanyika kesho katika Uwanja wa Taifa dhidi ya
Congo-Brazzaville.
Akiongea na waandishi wa habari leo
Jijini Dar es Salaam Mhe.Nape amesema milango ipo wazi kwa wadau wengine wa
michezo kujitolea katika kuiwezesha timu na hivyo kufanya vizuri katika
mechi hii ambayo ni muhimu sana kushinda ili kufuzu kwa fainali hizo.
“Hii timu ni yetu sote hivyo
inahitajika tuimiliki, tuepe nguvu, tuiombee ili iweze kufanya vizuri na
hatimaye kufuzu kuingia fainali kwa kuitoa timu ya Congo-Brazzaville” alisema
Mhe. Nape.
Aidha aliongeza kuwa kesho asubuhi
atakutana na wachezaji wa timu hiyo ili kuwapa maneno ya faraja kabla ya kuanza
kwa mechi na kuwataka watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwapa
motisha wachezaji kwa kuwashangilia na kuwatia moyo.
Mbali na hayo Waziri Nape alitoa
ufafanuzi kuhusu matumizi ya kadi za kieletroniki zilizozinduliwa hivi karibuni
kwa kueleza kuwa kadi hizo bado hazijaanza kutumika rasmi ili zitaanza kutumiwa
katika mchezo baina ya Wabunge wa Simba na Yanga pamoja na Bongo Fleva.
Timu ya Serengeti Boys inaundwa na
vijana wa Kitanzania wenye umri chini ya miaka 17 ambapo katika mchezo wa kesho
watahitaji ushindi na baadaye kufanya mechi ya marudiano mnamo Oktoba 2 mwaka
huu nchini Congo-Brazzaville.
No comments