Breaking News

BUKOMBE YATEKELEZA ILANI YA CCM KWA KISHINDO

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati - Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameupongeza uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukombe kwa Mkutano Mkuu Maalum wa kutoa taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM Jimbo la Bukombe kwa mwaka 2020-2025.

Rais Mstaafu Kikwete ametoa pongezi hizo leo Februari 8, 2025 wakati akihutubia katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika katika Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita.

“Nawapongeza kwa kuandaa Mkutano huo kwa kuwa unakidhi takwa la katiba ya CCM kwa kuwa inawezesha kupima mlipotoka, mlipo na mnapokwenda. Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 1977 toleo la 2022 katika Ibara ya 72 (1) inatambua kuwa Mkutano Mkuu ni kikao kikubwa cha Chama katika ngazi ya wilaya, aidha Ibara ya 74 imetamka kazi za msingi za Mkutano huu kuwa ni kuzungumza mambo yote yanayohusu ulinzi na usalama na maendeleo kwa ujumla katika wilaya.”Amesema Rais Kikwete.

Ameendelea kwa kuwasihi wanachama wa CCM kudumisha umoja na mshikamano “Wekeni mbele maslahi ya Chama chetu, watajitokeza watu mbalimbali kuja kugombea nafasi mbalimbali wapokeeni lakini wakitokea wenye maneno tu waambieni sie tunataka maendeleo sio maneno"

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM Bukombe amempongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi zilizosaidia utekelezaji wa idadi kubwa ya miradi ya maendeleo katika Jimbo hilo.
“Nyie wenyewe mmeona yaliyofanyika Bukombe ni mengi sana na hakuna mkoa wilaya au jimbo ambalo halikuguswa na Rais Samia. Hii ndio sababu ya msingi iliyofanya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika Dodoma Januari mwaka huu kumchagua kuwa mgombea wa chama chetu kwa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,” amesema Rais Kikwete.

Amebainisha kuwa miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa inaonekana na ina faida kwa wananchi huku akieleza jitihada za Dkt. Biteko za kuleta maendeleo katika Jimbo hilo. “ Naomba kuwahakikishia kuwa hamkufanya makosa kumpa kura zenu Dkt. Biteko, naomba niwaambie kuwa mambo haya mazuri ya Bukombe yasingetokea kama msingemchagua Dkt. Biteko.”

Aidha, Rais Kikwete amewaasa wananchi wa Bukombe kuwachagua wagombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ili kuendeleza miradi ya maendeleo katika Jimbo hilo.

Katika hatua nyingine, Rais Mstaafu Kikwete amemshukuru na kumpongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mzuri wa nchi na kuwa nchi imetulia na ina amani na maendeleo yanaonekana katika kila eneo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi Bukombe kwa mwaka 2020 - 2025 amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo. 

“Nianze kwa kusema kwa yote yaliyotekelezwa katika Jimbo hili yametokea kwa sababu ya matashi mema ya Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatupenda sana wananchi wa Bukombe, kwa kipindi ambacho nimekuwa mbunge nimeona ametoa fedha nyingi sana kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Jimbo leo,” amesema Dkt. Biteko. 

Vilevile, amesema kuwa Rais Samia ameridhia ujenzi wa barabara ya kutoka Ushirombo hadi Katoro kwa kiwango cha lami na kuwa mkandarasi anatafutwa kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Ameongeza kuwa Wilaya ya Bukombe inatarajia kutekeleza mradi mkubwa wa nishati ya umeme katika Kata ya Busonzo ambao utazalisha megawati 5 zitakazoingizwa katika gridi ya Taifa.
Awali akiwasilisha taarifa ya miradi ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa njia ya makala ya picha jongefu, Dkt. Biteko ametaja miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu, huduma za afya, maji, usambazaji wa nishati, ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara na matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari.

Katika sekta ya nishati, makala hiyo inaeleza kuwa huduma ya usambazaji umeme imefika katika vijiji vyote 64 vya Jimbo hilo ili kuendelea kukuza fursa za uwekezaji na kukuza uchumi kwa wananchi. 

Katika sekta ya elimu, sehemu ya makala hiyo inataja miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Bulumbaga wenye gharama ya Sh. 40,000,000.00; ujenzi wa vyumba nane vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Msonga- Ikuzi (Mpya) wenye gharama ya Sh. 160,000,000.00 na ujenzi wa matundu ya vyoo ishirini na nane katika shule ya msingi Msonga wenye gharama ya shilingi milioni 47,439,000,00.

Aidha, katika sekta ya afya, ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na uboreshaji wa hospitali ya wilaya umesaidia kuboresha huduma za afya katika hospitali na kuboresha hali za afya za wananchi kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ukamilishaji wa Zahanati ya Kagwe kwa gharama ya Sh. 50,000,000.00., ukamilishaji wa Zahanati ya Lyambomgongo kwa gharama ya Sh. 50,000,000.00 na ujenzi wa Zahanati ya Ishololo kwa gharama ya Sh. 101,223,889.86.
Aidha, miradi mingine iliyotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao ya kilimo Msangila kwa gharama ya Sh. 993,314,906.24, uchimbaji wa kisima kirefu katika kijiji cha Namonge Sh.16, 348,900.00 na matengenezo ya sehemu korofi katika barabara ya Uyovu - Namonge – Namarandula (1.50Km) kwa gharama ya Sh. 90,161,000.00.

Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amewashukuru madiwani wote wa Jimbo lake kwa kusimamia vizuri miradi ya maendeleo katika maeneo yao huku akiwahakikishia kuendelea kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi wao.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella amempongeza Rais Mstaafu Kikwete kwa jitihada alizofanya wakati wa uongozi wake kwa kujenga msingi mzuri wa kuhakikisha watoto wanapata elimu nchini.

“ Katika uongozi wa Rais Samia tumejenga shule mpya 150 na wakati ule unatengeneza Ilani Mhe. Rais Kikwete uliona mzigo kwa wazazi kusomesha watoto na sasa katika uongozi wa Rais Samia kila mwezi tutapokea shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kusomesha watoto,” amesema Mkuu wa Mkoa Shigella.

Ameongeza “ Rais Samia ametuleta magari 15 ya kubeba wagonjwa mahututi ambayo tumeyagawa katika hospitali zetu na vituo vya afya. Mkoa wetu pia umepata zaidi ya dola milioni 165 zitakazosaidia kupeleka maji Chato, Wilaya ya Geita na vijijini, hivyo kufikia malengo ya Serikali ya kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa jamii.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe, Matondo Luhonja amesema kuwa Mbunge wa Bukombe, Dkt. Biteko amekuwa kiongozi msikivu, makini na mwenye ushirikiano na wananchi wake na hivyo mafanikio hayo ya utekelezaji yamechangiwa pia na uongozi wake mzuri.

Mkutano huo Mkuu wa CCM Bukombe umehudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Bukombe uliambatana na burudani kutoka kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya Harmonize.

No comments