MEGAWATI 30 ZA JOTOARDHI KUINGIA KWENYE GRIDI IFIKAPO 2026/2027 - DKT KAZUNGU
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt. Khatibu Kazungu akizungumza kwenye mkutano mkuu wa muunganiko wa nchi kwenye masuala ya jotoardhi una iendelee mjini Abu Dhabi
Abu Dhabi, UAE - Imeelezwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye rasilimali kubwa ya uwekezaji miradi ya jotoardhi ambapo jumla ya megawati 30 zinatarajiwa kuingizwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwaka 2026/2027
Hii inafuatia uwepo wa Megawati 5000 za umeme na Megawati 15000 za Joto Kwa ajili ya matumizi ya Moja Kwa moja kwenye miradi ya jotoardhi.
Hayo yameelezwa Januari 14, 2025 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia umeme na nishati jadidiifu Dkt Khatibu Kazungu wakati wa mkutano mkuu wa muunganiko wa nchi kwenye masuala ya jotoardhi yaani Global Alliance ambao umefanyika kwenye baraza kuu la 15 la IRENA.
📌 Anadi fursa za uwekezaji miradi ya Jotoardhi Baraza la 15 IRENA
📌 Asema Tanzania ina maeneo 50 yenye vyanzo vya Jotoardhi
📌 Ngozi, Kiejombaka, Songwe na Luhoi yatajwa kuwa miradi ya kimkakati uzalishaji Jotoardhi
Kazungu amesema kuwa Tanzania inatarajia kuwa miongoni mwa nchi ambazo zinaongoza kwenye uendelezaji wa umeme wa jotoardhi Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Akinadi fursa ziilizoko nchini Tanzania katika mjadala wa ngazi ya juu kwenye mkutano huo, Dkt Kazungu amesema rasilimali hiyo ya jotoardhi inachagizwa na uwepo wa mikondo miwili ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki ambacho ndicho chanzo kikuu Cha Nishati hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
‘’Tanzania imeainisha maeneo 50 ambayo yana viashiria vya uwepo wa rasilimali ya jotoardhi katika mikoa takribani 16 ya nchi yetu, maeneo hayo yapo katika hatua mbali mbali za uendelezaji kwa ajili ya uzalishaji umeme na fursa ya matumizi ya moja Kwa moja.’’ Amesema Dkt Kazungu
Aidha ameongeza kuwa Tanzania inawakaribisha wabia wa maendeleo, taasisi binafsi kuwekeza Tanzania ili kuweza kuchangia upatikanaji wa nishati safi ya uhakika, endelevu na rafiki wa mazingira
Aidha amesisitiza kuwa pamoja na uwepo wa vyanzo hivyo, pia serikali kupitia kampuni ya Uendelezaji Joto Ardhi Tanzania TGDC ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO, imetoa kipaumbele Kwa miradi mitano ya kimkakati ili kuweza kuharakisha upatikanaji wa nishati hiyo, miradi hiyo ni pamoja na ule wa Ngozi-MW 70, Kiejo mbaka 60MW iliyopo mkoani Mbeya, Songwe-MW 38 iliyopo mkoani Songwe na Luhoi-MW 5 iliyopo mkoani Pwani, ambapo Miradi hii ipo katika hatua ya uhakiki wa rasilimali ,na Mradi wa Natron wa Megawati 60 mkoani Manyara ambao upo katika hatua ya utafiti wa kina.
Ameongeza kuwa pindi niradi hiyo itakapoanza kuzalisha umeme itachagiza uchumi wa nchi, kutunza mazingira na kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja kupitia upatikanaji wa ajira.
Amesema kwa sasa Tanzania inajipanga kuhakikisha miundombinu, ushirikishwaji wa sekta binafsi na wabia wa maendeleo wanapewa kipaumbele kwenye utekelezaji wa miradi hii ambayo ni rafiki kwa mazingira.
No comments