FCC YAZINDUA WIKI YA USHINDANI 2024
Dar es salaam - Tume ya Ushindani nchini (FCC) imezindua wiki ya ushindani kitaifa huku wakijipanga kutumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wadau kutoka sekta mbalimbali nchini wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu na wanasheria ili kujiepusha na vitendo ambavyo vinarudisha nyuma ushindani na maendeleo ya Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam wakati akizindua wiki ya ushindani, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) William Erio, amesema katika kusherekea siku muhimu ya ushindani duniani inayoadhimishwa Disemba 5 kila mwaka ambapo watakutana na kufanya semina na wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu na kufanya vipindi vya kuelimisha umma kupitia kwenye runinga na redio ili watanzania waweze kuelimika na kunufaika na elimu itakayotolewa.
Amesema kuwa wadau wote watakaokutana nao watapewa elimu na kuwajulisha FCC inafanya nini,serikali yao inafanya nini katika kuhakikisha kwamba sera na sheria za ushindani zinaondoa hali yoyote inayoondoa usawa sokoni na kurudisha nyuma maendeleo ya ushindani nchini.
“Tunazindua leo shughuli yetu na kuanzia siku ya jumatatu tarehe 02 na 03 December tutafanya semina kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na wanasheria ili kuwaeleza kwa kina kuhusu siku yetu hii tukijikita katika kauli mbiu yetu na siku ya tarehe 04 December tutatoa elimu kwa umma kupitia runinga na redio ambapo kilele cha maadhimisho yetu haya yatakua December 05 mwaka huu”
Bw. Erio amesema kuwa FCC wana wajibu wa kuwakumbusha wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa kuzingatia kanuni na taratibu pamoja na misingi ya ushindani na kuwaelimisha wananchi kuhusu serikali yao nini inafanya katika kuhakikisha inawalinda.
Amesema kupitia maadhimisho hayo wao kama taasisi wataonyesha namna walivyojipanga katika kuhakikisha wanaboresha mifumo na utendaji wao jambo ambalo litasaidia utekelezaji wa majukumu yao yawe mazuri zaidi na kuyawezesha makampuni na wafanyabiashara wa Tanzania kunufaika na fursa zilizopo katika soko huru la biashara la afrika na lile lililopo katika jumuiya ya afrika mashariki.
Ameongeza kuwa siku ya ushindani duniani imelenga kuelimisha jamii, wadau kutoka sekta mbalimbali kuhusu kuzingatia umuhimu wa kanuni,sera na sheria za ushindani za biashara za hapa nchini na duniani kote.
“Kanuni za biashara zinawafanya watendaji wa biashara kuwa na fursa sawa kwa wote, na sheria zetu zipo katika mambo kadhaa ambayo yanazuia vitu ambavyo vitarudisha maendeleo ya kufanya biashara” amesema Bw. Erio.
Amesema kuwa vitu ambavyo sheria inakataza ni pamoja na kupanga bei za bidhaa wanazofanya, kupunguza uzalishaji, kugawana zabuni pamoja na kula njama ambayo itapelekea kurudisha nyuma maendeleo ya ushindani.
Moja ya majukumu makubwa ya FCC ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji, usambazaji na ugavi wa bidhaa na huduma katika kuhakikisha mazingira sawa ya ushindani wa soko baada ya nchi kuondokana na mfumo wa uchumi hodhi na kuhamia katika mfumo wa uchumi wa soko huria kwa maslahi mapana ya Taifa.
Maadhimisho ya wiki ya ushindani ya mwaka 2024 yanaongozwa na kauli mbiu : Sera ya ushindani inavyoweza kutumika katika kupunguza utofauti wa usawa katika ufanyaji biashara huku Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Jaffo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi siku ya Kilele cha maadhimisho hayo Disemba 5, 2024 yatakayofanyika Jijini Dar es Salaam.
No comments