Breaking News

INDIA YATAFUTA FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI TANZANIA

Kutokana na utajiri wa Rasilimali Madini ambayo nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa nayo yakiwemo madini ya Metali ,Vito , Viwandani , Madini ya kuzalisha Nishati pamoja na Madini adimu yameivutia Taifa la India kutafuta fursa za uwekezaji nchini Tanzania.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 3, 2024 na Balozi wa India nchini Tanzania, Balozi Bishwadiq Dey katika kikao cha kujadili fursa za uwekezaji katika sekta ya madini baina ya India na Tanzania.
Akizungumza na Naibu Waziri wa Madini- Tanzania Dkt.Steven Kiruswa, Balozi Dey amebainisha kuwa, India imetilia mkazo uwekezaji katika sekta ya madini Tanzania kama njia ya kujihakikishia upatikanaji wa rasilimali madini na kufungua fursa za uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.

Aidha, Balozi Dey , ameipongeza Tanzania kwa kufanya utafiti wa kina kwa asilimia 16 na kuongeza kuwa India inalenga kuongeza ushirikiano kwenye teknolojia, utafiti na ubunifu wa viwanda hususan katika uchenjuaji na uongezaji thamani madini ambao utaleta mageuzi katika mnyororo mzima wa thamani madini kwa pande zote mbili.

Balozi Dey ameongeza kuwa, pamoja na mambo mengine, India ina wataalam wengi katika maeneo ya Uongezaji thamani madini ,utafiti wa madini, ugani, uchorongaji na uchenjuaji madini hivyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuwajengea uwezo wataalam kwenye mnyororo mzima wa thamani madini nchini Tanzania.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini-Tanzania Dkt.Steven Kiruswa amefurahishwa na Taifa la India la kutafuta fursa za uwekezaji katika sekta ya madini nchini Tanzania na kuwa, Tanzania na India kwa kipindi kirefu zimekuwa na ushirikiano katika sekta mbalimbali.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa Tanzania inaendelea kutafuta wawekezaji wa kimataifa katika sekta ya madini ili kuweza kufikia malengo ya uchumi wa viwanda na ustawi wa Taifa kwa kuzingatia vipaumbele vya sekta ya madini kama vilivyoorodheshwa katika maono ya Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri.

Kikao hicho kimejumuisha wataalam kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ikiwemo Tume ya Madini , Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Ofisi ya Kamishna wa Madini ambapo kwa pamoja wametoa miongozo ya namna ya kupata taarifa za madini , miongozo ya kisheri na machapisho ya fursa za madini zilizopo nchini.



No comments