Breaking News

WAKUU WA MIKOA NA WILAYA SIMAMIENI UBAINISHAJI WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM

OR-TAMISEMI ARUSHA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mohamed Mchengerwa amewaagiza  wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha  wanasimamia zoezi la ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kupata fursa ya elimu.

Akifungua maadhimisho ya miaka 30 ya elimu jumuishi  Patandi Jijini Arusha Mhe. Mchengerwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama kufuatlia wazazi wanaowaficha watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kupata elimu kama stahiki ya mtoto wa Kitanzania.
“Nawaelekeza Viongozi wote wa Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia zoezi la ubainishaji na utambuzi wa awali wa watoto kwa wakati ili kubaini wenye mahitaji maalumu, kuwahimiza na kuhakikisha wazazi na walezi wanawapeleka watoto wao katika shule zilizoshauriwa na wataalamu ili wakaandikishwe na kuanza masomo na taarifa ya utekelezaji wake itolewe” amesema  Mhe. Mchengerwa.

Mchengerwa amesema hadi kufikia mwaka 2020 kulikuwa na wanafunzi wenye mahitaji maalumu 28,482 lakini idadi hiyo imeongezeka mpaka wanafunzi 78,429 mwaka 2024 na Serikali imetenga jumla ya shule 6,088 zinazopokea wanafunzi hao na kuwapatia afua stahiki ambapo shule takriban 309 zina mabweni kwa ajili ya wanafunzi hao.
Naye Dkt. Magreth Matonya, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Maalumu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia amesema malengo ya maadhimisho hayo ni kutangaza fursa za wanafunzi wenye mahitaji maalum zinazotolewa na Serikali, kutangaza mafanikio yaliyopatikana, kutoa elimu ya uhamasishaji na pia kufanya tathmini ya elimu jumuishi. 

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Maafisa Elimu wa Mikoa, Maafisa Elimu Watu Wazima Mikoa yote, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Elimu Msingi na Sekondari, Maafisa kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maafisa Elimu Maalum wa Halmashauri na Wadau mbalimbali wanaoihunga mkono Serikali.





No comments