Breaking News

UJENZI WA BARABARA YA IRINGA-MSEMBE KUFUNGUA UTALII NYANDA ZA JUU KUSINI

Na Happiness Shayo - Iringa 
Ujenzi wa Barabara ya Iringa - Msembe (km 104) kwa kiwango cha lami uliogharimu takribani shilingi bilioni 142.56 utasaidia kukuza utalii wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hasa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa kurahisisha ufikaji wa watalii katika hifadhi hiyo.

Hayo yamesemwa leo Septemba 21, 2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) wakati wa hafla ya Utiaji Saini Mikataba ya Ujenzi na Usimamizi wa Barabara ya Iringa-Msembe kiwango cha lami iliyofanyika leo Septemba 21,2024 katika Uwanja wa Samora, Mkoani Iringa.

“Ujenzi wa barabara ya hii pamoja na mambo mengine utasaidia kuongeza idadi ya watalii na hasa Utalii wa ndani na kukuza pato la Taifa, haya ni mafanikio makubwa kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.” amesisitiza Mhe. Chana.

Ameongeza kuwa mradi huo pia utasaidia kufungua fursa za upatikanaji wa huduma za kijamii na kukuza uchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa huku akiwataka wawekezaji kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Hifadhi mbalimbali za Nyanda za Juu Kusini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) amesema Barabara hiyo pamoja na mambo mengine itatoa mchango mkubwa katika shughuli za utalii kwenye Hifadhi ya Taifa Ruaha iliyopo Mkoani Iringa.

"Utalii ili uweze kustawi lazima miundombinu iwepo hivyo barabara hii itakuza utalii ikiwa ni fedha ambazo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha kujengwa kwa Barabara hii" amesema.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Wabunge wa Mkoa wa Iringa, Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, Watendaji na Watumishi wa Taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Iringa.



No comments