DAR KUADHIMISHA SIKU YA AMANI SEPT 23, 2024
Mkoa wa Dar es Salaam umepanga kuadhimisha siku ya Amani Duniani, Sept 23,2024.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt Toba Nguvila amesema Maadhimisho ya Amani Duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 21 Septemba, kwa lengo la kuhamasisha watu wote Duniani kuzingatia umuhimu wa Amani katika jamii zao.
Siku hii inatumiwa kuwakumbusha watu kuhusu umuhimu wa kutatua migogoro kwa njia za Amani, kuzuia vita, kuimarisha mshikamano na umoja miongoni mwa watu wa mataifa mbalimbali.
Vilevile ni fursa ya kuangazia masuala ya haki usalama na maendeleo endelevu ili kujenga Dunia bora kwa kila mtu.
Aidha Dkt Nguvila amesema maadhimisho ya siku hii ya Amani yanatoa fursa kuhamasisha watu kuhusu misingi ya Amani, kukabiliana na migogoro, kujenga uelewa na kujitolea kwa jamii.
Sambamba na hilo Dkt Toba amesema kwa kutambua umuhimu wa Amani katika Taifa letu, Mkoa umepanga kufanya maadhimisho haya tarehe 23 septemba 2024 katika viwanja vya Leaders Club Wilaya ya Kinondoni kuanzia saa 1:00 asubuhi, ambapo amesema kutakuwepo na shughuli mbalimbali ikiwemo hotuba za viongozi wa Dini, burudani, Sanaa mbalimbali, michezo na maonyesho yanayoonyesha umuhimu wa Amani.
Mwisho Katibu Tawala Mkoa amewakaribisha wananchi wote, bodaboda, Mama Lishe, Machinga, Vyama vya Siasa na Asasi za Kiraia kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Leaders ili kushiriki Maadhimisho haya ya siku ya Amani
“Dumisha Amani, Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”
No comments