Breaking News

KAYA 58 ZENYE WANANCHI 228 NA MIFUGO 350 ZAHAMA HIFADHI YA NGORONGORO

Na Mwandishi wetu, Ngorongoro.
Katika muendelezo wa hamasa ya wananchi wa Ngorongoro kujiandikisha kuhama kwa hiari, leo tarehe 7 Septemba, 2024 jumla ya kaya 58 zenye wananchi 228 na mifugo 350 wamehama katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera na maeneo mengine waliyochagua katika wilaya za Monduli, Meatu na Simanjiro.

Akitoa taarifa wakati wa kuaga kundi la 19 la awamu ya pili linalohama kutoka hifadhi ya Ngorongoro, Meneja mradi wa kuhamisha wananchi wa Ngorongoro Afisa Uhifadhi Mkuu Flora Assey ameeleza kuwa, kati ya kaya  58 zilizohama leo, kaya 30 zenye watu 151 na mifugo 235 zinahamia Kijiji cha Msomera,  Kaya 28 zenye watu 78 na mifugo 115 zinakwenda maeneo mengine waliyochagua katika wilaya za Monduli Mkoani Arusha,  Meatu mkoani Simiyu na Simanjiro katika mkoa wa Manyara.

Amebainisha kuwa tangu zoezi la kuhamisha wananchi kwa hiari lilivyoanza mwezi Juni 2022 hadi kufikia leo Septemba 7, 2024 Jumla ya kaya 1,627 zenye watu 9,778 na mifugo 40,051 zimeshahama ndani ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro
Akiaga kundi hilo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Katibu tawala wa Wilaya hiyo Bw. Hamza Hussen Hamza ameeleza kuwa, muitikio wa wananchi kuendelea kuhama ndani ya hifadhi hiyo unasaidia kupunguza shughuli za kibinadamu hifadhini, kupunguza changamoto kwa wananchi wanazokutana nazo kwa kuishi na wanyamapori wakali na hatarishi, kukosa uhuru wa kumiliki vyombo vya moto na kufanya shughuli za kiuchumi pamoja na  kukosa uhuru wa kutembea ndani ya hifadhi baada ya saa 12 jioni.

“Tunawapongeza sana kwa maamuzi ya kuhama hifadhini kwa ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi, maeneo mnayohamia Serikali imeshawajengea huduma muhimu kama shule, zahanati, maji, majosho, mawasiliano, nishati ya umeme, makazi bora pamoja na mashamba ya kilimo na malisho. Pamoja na zoezi hili la kuhama kuendelea, niwahakikishie wananchi ambao bado hawajaamua kuhama kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma za kijamii na katika utekelezaji wa zoezi hili tutaendelea kuzingatia misingi ya sheria, kanuni, taratibu na haki za binaadamu” aliongeza Hamza.
Mwakilishi wa kamishna wa Uhifadhi NCAA, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia idara ya maendeleo ya Jamii, Gloria Bideberi ameainisha kuwa, Serikali kupitia NCAA inaendelea na zoezi la kuelimisha, kuandikisha na kuhamisha wananchi wanaohama kwa hiari na kuongeza kuwa mwananchi anayejiandikisha akishathaminishiwa mali zake, taratibu za malipo hufanyika kwa muda mfupi na ndani ya wiki mbili mwananchi husika anahamishwa kutoka ndani ya hifadhi.

Kamishna Bideberi ameongeza kuwa sambamba na zoezi la kuhamisha wananhi wanaojiandikisha kuhama kwa hiari, shughuli za uhifadhi na utalii zinaendelea vizuri, maeneo wananchi waliyohama tayari uoto wa asili umeanza kurejea na wageni kutoka ndani na nje ya nchi wanaendelea kutembelea kwa wingi vivutio vya utalii vilivyoko katika hifadhi hiyo. 
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wanaohama kwa hiari, Elizabeth Saiboko kutoka Kijiji cha Nainokanoka amebainisha kuwa ameamua kuhama ndani ya hifadhi ili kuwa huru zaidi na kutafuta kesho iliyobora kwa watoto wake kwa kuwa katika tarafa ya Ngorongoro sheria za uhifadhi zinauiya baadhi ya shughuli za kiuchumi kama kilimo, ujenzi wa nyumba za kudumu, kumiliki vyombo vya moto na uhuru wa kutembea  kwa saa 24 tofauti na maeneo mengine nje ya hifadhi.


No comments