WAZIRI UMMY; NI MUHIMU KUWEKEZA KATIKA KUITUNZA NA KUILINDA AFYA
Afya ni mtaji bora zaidi duniani, ni muhimu kuwekeza katika kuilinda na kuitunza afya yake kwa kuepuka mtindo mbovu wa maisha kwani kwa kiwango kikubwa huchangia janga la magonjwa yasiyoambukiza [NCD's].
Akizungumza mara baada ya kuhitimika kwa matembezi ya hisani [Walk the Talk] yaliyoratibiwa na Shirika la Afya Duniani [WHO Tanzania] Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika elimu ya afya kwa Umma juu ya kulinda afya zao kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.
"Tutaendelea kuwekeza katika elimu ya afya kwa Umma, [kuhimiza jamii] ilinde afya zao ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza kwani kinga ni bora kuliko tiba," Alisema Waziri Ummy.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa kumekuwepo na wagonjwa wengi hasa wenye Shinikizo la Juu la Damu na Kisukari nchini na kubainisha kuwa Kama kweli tunataka Afya zetu ziwe salama lazima kila mmoja aanze kuchukua hatua ili tuepuke magonjwa yasiyoambukiza.
Alisema Takwimu za mwaka 2023 za Wizara ya Afya zinaonesha kiwa magonjwa hayo mawili yaliyo katika kundi la magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakizidi kushika kasi kwa kuwa na idadi kubwa.
Kulingana na ripoti hiyo, magonjwa hayo kwa mara ya kwanza yameingia katika orodha ya magonjwa 10 yanayoongoza kwa rekodi ya idadi kubwa ya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Waziri Ummy ameihimiza jamii kuepuka tabia bwete na mtindo mbovu wa maisha ili kuepukana na magonjwa hayo.
"Tunahitaji kuwekeza katika afya, vijana zingatieni mtindo bora wa maisha, ulaji unaofaa na kujenga desturi ya kufanya mazoezi," amesema.
Amesisitiza ni muhimu kuwekeza katika afya kwani magonjwa yasiyoambukiza yana gharimu uchumi katika kuyagharamia, yakiathiri wengi na hata kusababisha vifo.
Pamoja na hayo amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za makusudi za kuwekeza kwenye miundombinu ya kutoa huduma za Afya.
"Ikiwemo kujenga Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za ngazi zote na kuimarisha upatikanaji wa huduma za uchunguzi ikiwemo huduma za maabara," amesema.
Post Comment
No comments