TUCHUKUE HATUA KUWEKEZA KWENYE AFYA ZETU - WAZIRI UMMY

Na WAF - Dar Es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kuchukua hatua katika kuwekeza kwenye Afya zao kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa Afya ikiwemo kufanya mazoezi ili kuepuka tabia bwete. 

Waziri wa Afya Ummy mwalimu amesema hayo leo Aprili 13, 2024 baada ya matembezi ya hisani ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya siku ya Afya Dunia yaliyoanzia katika ofisi za Shirika la Afya Dunia (WHO) hadi daraja la Tanzanite Jijini Dar Es Salaam. 
“Tumeona wagonjwa wengi wenye Shinikizo la Juu la Damu na Kisukari, kama kweli tunataka kuwekeza kwenye Afya zetu lazima kila mmoja aanze kuchukua hatua ili tuepuke magonjwa Yasiyoambukiza”. Amesema Waziri Ummy 

Amesema, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuchukua hatua za makusudi katika kuwekeza kwenye miundombinu ya kutoa huduma za Afya ikiwemo kujenga Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za ngazi zote pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma za uchunguzi ikiwemo huduma za maabara. Amesema Waziri Ummy 
“Lakini pia, Serikali inaendelea kuwekeza katika upatikanaji wa rasilimali watu wa Afya kwa ngazi zote kuanzia huduma za Afya za msingi hadi huduma za ubingwa na ubingwa bobezi, kuimarisha upatikanaji wa dawa pamoja na kuwekeza kwenye elimu ya Afya kwa Umma”. Amesema Waziri Ummy 

Aidha, Waziri Ummy amesema katika kila Watanzania 100, Nane tu ndio wana bima za Afya hali ambayo inapelekea kuelemewa kwa mifuko hiyo kwa kuwa ndio inaendesha Sekta ya Afya ikiwemo Hospitali za Serikali na Hospitali binafsi.
“Katika kufikia lengo la Afya kwa wote, Serikali inajikita katika kuhakikisha tunaimarisha mifuko ya bima ya Afya ikiwemo mfuko wa NHIF pamoja na mifuko ya Bima binafsi ili Watanzania wengi waweze kuwa na bima za Afya.” Amesema Waziri Ummy 

Waziri Ummy ametoa wito kwa makampuni ya Bima za Afya kuanzisha mipango ya kuwa na bima ya Afya kwa Watanzania ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi hasa wananchi wa kipato cha chini pindi wanapougua.

No comments