Breaking News

TUGHE YAIPONGEZA SERIKALI KWA KUKUBALI OMBI LA TUGHE LA KUANZA KULIPA POSHO YA MADARAKA

Dodoma 
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimefurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kuanza kulipa Posho ya Madaraka kwa Waganga Wafawidhi katika Vituo vya kutolea huduma za Afya ngazi ya msingi kama ilivyotangazwa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu (MB) jana tarehe 14 Februari 2024 Jijini Dodoma wakati akifunga Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wafawidhi wa Vituo vya kutolea huduma ya Afya ngazi ya msingi.

Akitoa pongezi hizo, Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Cde. Hery Mkunda ameeleza kuwa, kwa muda mrefu Chama cha TUGHE kimekuwa kikiwasilisha Serikalini hoja hii ya Posho ya Madaraka kwa  Waganga Wafawidhi katika vituo vya kutolea huduma ya Afya na kurejea kurejea Barua  ya tarehe 05/10/2023 iliyoandikwa na Ofisi ya Katibu Mkuu TUGHE kwenda Ofisi ya Rais -TAMISEMI) iliyokuwa na kichwa cha Habari (“Kuwasilisha Hoja na Changamoto za Watumishi wa Sekta ya Afya) ambayo ilieleza pia hoja hii hivyo TUGHE imefurahishwa sana na uamuzi huo na  kuipongeza Serikali kwa kukubali kuanza kulipa Posho hii kwa wataalamu hao muhimu kuanzia Julai 2024.

“Bado tunaendelea kuikumbusha Serikali kuendelea kushughulikia changamoto nyingine ambazo bado Watumishi wanakumbana nazo kama vile kama vile ajira za mikataba kwa baadhi ya Watumishi wa Umma, Nyongeza ya posho ya kuitwa kazini “On-call allowances” pamoja na changamoto ya Malipo ya nauli za likizo kwa Watumishi wasio Walimu katika Halmashauri za Wilaya kulipwa toka katika mapato ya ndani ya Halmashauri badala ya kulipwa moja kwa moja toka hazina kama ilivyo kwa waalimu, Changamoto za kutokamilika kwa Muundo wa Watumishi wa Mahakama” alisema Katibu Mkuu TUGHE

Aidha, TUGHE imeendelea  na majadiliano na wadau katika kuhakikisha Mama wanaojifungua Watoto njiti wanaongezewa siku zaidi za likizo ya uzazi. Sambamba na hayo pia Chama kitaendelea kuwasilisha mapendekezo mbalimbali Serikalini yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi ili kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini ili kuongeza tija na uzalishaji katika maeneo ya kazi.

Imetolewa na 
IDARA YA HABARI NA UHUSIANO KWA UMMA TUGHE

 

No comments