MADALALI WA NYUMBA NA VIWANJA KURASIMISHWA
Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa Mkutano Mkuu wa Wadau wa Sekta ya Milki Tanzania kuanzia Januari 19, 2023 hadi Januari 20.
Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambao ndio wanaoandaa mkutano huu inasema kaulimbiu ya mkutano wa wadau kwa mwaka huu ni "Urasimishaji wa Shughuli za Mawakala wa Milki (Madalali) kwa Maendeleo ya Taifa."
Kauli mbiu hii inalenga kutoa muongozo wa kutambulika rasmi kwa mawakala wa milki au kwa jina maarufu madalali wa nyumba na viwanja ili kuhakikisha kunakuwepo na soko imara na lenye uwazi kwa ajili ya kulinda wadau wa sekta ya milki nchini ambao ni wenye nyumba, wapangaji, madalali na taasisi za kifedha.
Urasimishaji wa madalali unaweza kuwa mojawapo ya njia za kufanikisha malengo ya kumaliza migogoro ya upangaji, ujenzi, ununuzi, uuzaji na upangishaji wa makazi kwa kuzingatia mahitaji ya kila mdau.
Wizara ya Ardhi imekamilisha maboresho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995. Pamoja na mambo mengine, sera hiyo itaweka utaratibu mahususi wa usajili wa mawakala wa milki nchini pamoja na kuanzisha chombo cha kusimamia sekta ya milki.
Source Global TV
Post Comment
No comments