Breaking News

ACT WAZALENDO YATOA MREJESHO AWAMU YA KWANZA YA MIKUTANO YA HADHARA

Waziri Mkuu Kivuli wa chama ACT Bi. Dorothy Semu akifafanua jambo wakati akiwasilisha mawasilisho ya awamu ya kwanza ya Mikutano ya Hadhara waliyofanya maeneo mbalimbali nchini makuu ya chama leo Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa  Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari wakati chama kikitangaza mrejesho wa majumuisho ya mikutano mara baada ya kuhitimisha awamu ya kwanza makao makuu ya chama leo Jijini Dar es Salaam

Dar es salaam:
Chama cha ACT Wazalendo kimesema kitaendelea na mikutano ya hadhara na kutangaza ya Brand Promise yake katika awamu ya pili ambayo itaanza Mei 4 hadi 13 mwaka huu katika mikoa 9 ya Tanzania bara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam kutoa mrejesho wa majumuisho ya mikutano mara baada ya kuhitimisha awamu ya kwanza Katibu Mkuu wa Chama hicho Ado Shaibu amesema ratiba ya mikutano ya hadhara ya awamu ya pili itaanzia mkoani Ruvuma na kumalizia mkoani Mwanza.

Anesema mikoa itakayofanyika mikutano hiyo kuwa ni Ruvuma, Njombe, Rukwa, Katavi, Mkoa wa Kichama Kahama, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mwanza.

Awali akitoa mawasilisho ya awamu ya kwanza ya Mikutano ya Hadhara waliyofanya maeneo mbalimbali nchini Waziri Mkuu Kivuli wa chama hicho Dorothy Semu amesema huduma duni za afya ni changamoto kwa wananchi.

Aidha amesema chama cha ACT Wazalendo kimeishauri Serekali ilete maboresho ya sheria kuhusu mifuko ya hifadhi ya jamii PSSF na NSSF ili wananchi watumie kupata huduma za afya kwa kuchangia elfu ishirini kwa mwezi na serikali ichangie elfu kumi.

“Watu wote wasiokuwa kwenye ajira rasmi hawana mfumo mzuri wa kuwalinda na kuwahakikishia wanapata matibabu, pensheni, likizo au mapumziko ya uzazi wala kulindwa kutokana na majanga, fao la kukosa kazi na hawana uwezo wa kuweka akiba kwa ajili ya baadaye” Amesema Bi. Semu na kuongeza kuwa,

“Athari za haraka zinazolikumba kundi kubwa la watanzania kwa kutokuwepo kwenye mfumo wa Hifadhi ya Jamii utaiona kwenye suala la matibabu, kote tulikopita tumekutana na vilio vya wananchi kuhusu gharama kubwa za matibabu, kukosekana kwa huduma bora hususani kwa wananchi vijijini na maskini. Takwimu zinasaidia kuonyesha kukosekana kwa usawa katika utolewaji wa huduma za afya nchini. Ni watanzania Milioni 9 (9,094,624) pekee kati ya watu Milioni 61 ndio wana uhakika wa matibabu kupitia Bima ya afya, kati yao wenye uhakika zaidi ni wale wenye Bima ya afya ya Taifa (NHIF) na Bima Binafsi ambao ni wastani wa watu Milioni 4.8”

Kuhusu migogoro ya ardhi amesema wimbi kubwa la wawekezaji kuchukua ardhi ya wananchi katika vijiji vya Muhoro, Ikwiriri ambapo wananchi wanataka kuhamishwa kupisha mwekezaji wa mashamba ya mpunga, Tarafa ya Makere vijiji vya Mvugwe na Kumtundu Wilaya ya Kasulu wamebomolewa makazi yao, kunyang’anywa ardhi zao na mashamba ili kupisha mwekezaji wa kiwanda cha Sukari bila kupewa fidia, bila kufuatwa kwa utaratibu wa ardhi za vijiji.

Aidha taasisi za Serikali kupora ardhi ya wananchi ambapo matukio ya namna hiyo yametokea Pwani, Mamlaka ya Bandari imepora ardhi ya wananchi zaidi 120 Kisiju ili Kujenga Bandari bila kutoa fidia tangu mwaka 2017. Wakala wa misitu (TFS) kuchukua ardhi ya wananchi maeneo ya Muhoro wilaya ya Rufiji, Mkoani Pwani kwa kuzuia mazao yao, kuwakamata vijana na kuwaweka vizuizini na wengine kujeruhiwa.

“Hali hiyo tumeikuta pia Kasulu, huko hali ni mbaya zaidi ambapo Serikali kupitia TFS imekuwa ikitoa kibali kwa wananchi kwenda kulima kwenye maeneo hayo lakini inapofika wakati wa mavuno, TFS na Askari na maliasili wanaenda kuvuna kwenye mashamba ya wakulima kupitia magari yao (kutaifisha) kwa madai ya kwamba wananchi wameenda kuvamia maeneo ya maliasili” Amesema Bi. Semu.

Aidha kuhusu fedha za TASAF amesema zitolewe kwa mujibu wa sheria sio kibaguzi na zisitumike kuwalaghai watanzania kwani ni mkopo wa world Bank na utalipwa kupitia kodi za watanzania hivyo waache kuwafanyisha wazee kazi ngumu ili walipewe fedha hizo.

Sambamba na hayo amesema mali asili za nchi ikiwemo Gesi zitumike kuondoa umaskini wa watanzania na serikali kujifunza kupitia uwekezaji walioingia usio na tija kwa wananchi na kuhakikisha kuwa wanaingia mikataba na wawekezaji ambayo itawanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo amesema lengo la chama ni kujenga uchumi wa wote kwa maslahi ya wote, unaozalisha ajira nyingi. Wananchi kumudu gharama za maisha na wawe na uhakika wa leo maisha ya kesho yao kwa kuwepo kwa mifumo ya pensheni kwa wote, afya kwa wote, akiba kwa wote, kuwanusuru kwenye majanga, kushuka kwa bei za mazao na mikopo nafuu.

No comments