CHAMA CHA SAU WAJA NA KAULIMBIU MPYA “SALA NA KAZI”
Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU) Bibi Bertha Mpata akifafanua jambo katika hafla ya uzinduzi wa kaulimbiu ya chama hicho itakayo tumika kuanzia leo hadi mwaka 2025.
Katibu Mkuu wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU) Bwana Majalio Kyara alizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kaulimbiu ya chama hicho itakayo tumika kuanzia leo hadi mwaka 2025.
Dar es salaam:
Chama cha Sauti ya Umma (SAU) kimezindua kaulimbiu yake mpya ya “Sala na Kazi” kitakayo kwenda nayo hadi mwaka 2025.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kaulimbiu hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Bi Bertha Mpata amesema lengo la kaulimbiu ni kuwafanya watanzania kuwa na hofu ya Mungu.
“Baada ya kufanya tafiti zetu, tumejiridhisha kwamba kwa sasa Watanzania wanatakiwa kuwa na hofu ya Mungu ndani ya mioyo yao tunaomba umma wa Watanzania tunapokuja na kaulimbiu hii watupokee,” Alisema Bi. Mpata
Mpata amebainisha kwamba wameamua kuja na kaulimbiu hiyo kwa kutambua kwamba Mungu ndiye msingi wa kila jambo kwenye jamii.
Amesema wanaamini kwamba kupitia kaulimbiu hiyo wanaenda wataikomboa jamii ya Watanzania.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama Taifa Majalio Kyara ameeleza kwamba kwa sasa ni muda muafaka wa kaulimbiu hiyo kuifikia jamii ya Watanzania.
Alisema kupitia kaulimbiu hiyo wanaamini watakwenda kuliponya Taifa, hivyo amesisitiza kwa kuwaomba Watanzania kuipokea.
“Tunapenda kutoa rai kwa watanzania kuipokea kaulimbiu hii kwani itasaidia katika kuhifadhi na kuzilinda Tunu za Taifa,” alisema Bw. Kyara.
Aidha amesema kwamba wao wataanza kufanya mikutano yao ya hadhara baada ya mifungo ya wakristo na waislamu mapema mwezi Mei mwaka huu.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha SAU Zanzibar Amour Haji Ali amesema kwamba anakwenda kuwaeleza kaulimbiu hiyo wanachama na wananchi kwa upande wa Zanzibar.
Ametoa wito kwa Watanzania kila mmoja kwa imani yake kumuogopa Mwenyezi Mungu ili ifanikiwe.
No comments