Breaking News

WENYEVITI NA WASAJILI WA MABARAZA SIAMIENI MAADILI YA WANATAALUMA - WAZIRI UMMY

Na WAF - Dodoma
Wenyevyiti na Wasajili wa Mabaraza na Bodi za Kitaaluma nchini wametakiwa kusimamia maadili ya wanataaluma ili kulinda jamii na huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kikao cha pamoja na Wenyeviti wa Mabaraza ya kitaaluma na Bodi za ujasili zilizo chini ya Wizara ya afya kilichofanyika jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema viongozi hao wanao wajibu mkubwa wa kusimamia Maadili ya wanataaluma ili kuilinda jamii na huduma zinazotolewa kwa wananchi kwa kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kiwango kinachofaa na ni salama.

"Serikali chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika miundombinu ya afya na kuboresha mazingira ya kutolea huduma pamoja na kutoa ajira kwa watoa huduma za afya kote nchini".

"Kwa msingi  huu mna nafasi kubwa sana ya kuisaidia Wizara ya Afya katika kipaumbele kikubwa mwaka huu yaani kuongeza ubora wa huduma za afya nchini". Alisisitiza Waziri Ummy.

Hata hivyo Waziri Ummy hakusita kuzungumzia malalamiko ambayo wananchi wamekua wakitoa kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, wananchi mmoja mmoja na kupitia mifumo ya kutoa mrejesho wa Wizara ya Afya.

Ameongeza kuwa wananchi wamekua wakielekeza malalamiko yao kwa wanataaluma mbalimbali juu ya huduma mbaya, kukiuka Maadili ya kitaaluma na kutojaliwa wagonjwa na hata wanaotoa huduma.

"Tumeshuhudia malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kwenye vituo vya umma na hata kutoka kwenye hospitali binafsi, nawashukuru pale mlipofuatilia malalamiko hayo maeneo mbalimbali ya nchi yetu ili kubaini makosa na kuchukua hatua stahiki". Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy aliwasisitiza wenyeviti na wasajili hao kutoa adhabu kali sana kwa wale wachache wanaokaidi miiko na kanuni za maadili yao.

"Msiwaonee aibu, malalamiko haya yanapozidi wananchi watakata tamaa na kuikosa imani kwa Serikali yao ambayo imefanya juhudi kubwa kusogeza huduma za afya kwa wananchi". Alisisitiza Waziri Ummy.

Aliongeza kuwa wananchi wana haki ya kupata huduma bora, na kuwataka wanataaluma watambue hilo na kutimiza wajibu wao kwa moyo wa upendo bila kusukumwa au kuona wanawatendea hisani wateja wao. 

"Mtoa huduma yeyote awe kwenye vituo binafsi ama ya serikali  ana wajibu huu na wala sio hisani. Naagiza mkasimamie hili ili wanataaluma waelewe na wapende kutimiza wajibu huu bila shuruti".

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ametoa wito kwa Wenyeviti na Wasajili wa Mabaraza na Bodi  kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na magonjwa mbalimbali.


 

No comments