Breaking News

WAZIRI UMMY AZITAKA HOSPITALI ZA SERIKALI KUJIFUNZA KWA JKCI KWA KUTOA HUDUMA BORA

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kizungunza na wafanyakazi wa Hospitali ya JKCI Dar Group alipotembelea kuangalia utoaji wa huduma na mwelekeo wa Hospitali hiyo baada ya kuikabidhi kuwa chini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tangu mwezi Novemba 2022.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akifafanua jambo mara baada ya ziara ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akitembelea Hospitali ya JKCI Dar Group kuangalia utoaji wa huduma na mwelekeo wa Hospitali hiyo baada ya kuikabidhi kuwa chini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tangu mwezi Novemba 2022.

Hospitali za Serikali nchini zimetakiwa kuiga mfano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutokupokea rushwa kwa wagonjwa wanaowahudumia kwani wagonjwa wanahaki ya kupatiwa huduma hizo.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipotembelea Hospitali ya JKCI Dar Group kuangalia utoaji wa huduma na mwelekeo wa Hospitali hiyo baada ya kuikabidhi kuwa chini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tangu mwezi Novemba 2022.

Mhe. Ummy alisema Hospitali za Serikali kuanza ngazi ya Wilaya zinapaswa kuwa na mtazamo kama wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwani wao ni kazi tu, huwezi sikia hata siku moja mgonjwa ameombwa rushwa katika Taasisi hiyo. 

“Sijawahi katika miaka yangu sita ya uwaziri wa afya kupata malalamiko ya wananchi kusema wamedaiwa rushwa JKCI, wafanyakazi wa JKCI Dar Group msije mkaharibu taswira ya JKCI makao makuu, malalamiko yao ninayoyapata huwa ni ya gharama kubwa za matibabu jambo ambalo haliwezi kuepukika kwa huduma za matibabu ya moyo”, alisema Mhe. Ummy

Aidha Mhe. Ummy ameutaka uongozi wa JKCI kusimamia Hospitali ya JKCI Dar Group kujikita katika kutoa huduma za matibabu bobezi ya magonjwa ya moyo kwa watoto wenye umri chini ya miaka 15 na kuifanya JKCI makao makuu kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo watu wazima.

Mhe. Ummy alisema mwezi Novemba 2022 Serikali kupitia Wizara ya Fedha na msajili wa Hazina ilifanya uamuzi wa kuichukua Hospitali ya Dar Group na kuipa Wizara ya Afya ili iweze kuisimamia na kuiendesha ambapo Wizara iliona uhitaji wa matibabu ya magonjwa ya moyo nchini kuongezeka na kuamua kuiweka chini ya JKCI kupanua wigo wa huduma za matibabu ya moyo.

“Hospitali ya JKCI Dar Group ilikua Hospitali iliyojengwa kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wafanyakazi wa viwandani na kuendeshwa na watu wa vyama vya wafanyakazi ambapo ilisajiliwa na msajiri wa Hazina Wizara ya Afya kama Taasisi ya umma.

“Nafurahi kuona kwa kipindi cha miezi miwili baada ya kuikabidhi JKCI Hospitali hii ya JKCI Dar Group idadi ya wagonjwa imeongezeka lakini pia JKCI imeweza kurekebisha huduma za wagonjwa wa dharura kwa kipindi cha muda mfupi haya ni mafanikio makubwa na ya haraka”, alisema Mhe. Ummy

Mhe. Ummy ameutaka uongozi wa JKCI kuweka mazingira mazuri ya kuvutia ili JKCI Dar Group kuwa kituo cha umahiri wa matibabu ya moyo kwasababu Hospitali hiyo ipo katikati ya mji ambapo inauwezo wa kupokea wagonjwa kutoka Wilaya ya Temeke, Ilala, Kinondoni na wagonjwa wanaotoka nje ya nchi kwa urahisi kutokana na kuwa karibu na Uwanja wa ndege.

“Kutokana na mahali hospitali hii ilipo siwakatazi kutoa huduma za matibabu shirikishi kwani mgonjwa wa moyo anaweza akafika hospitali akiwa na tatizo la kichwa, tatizo la homa na matatizo mengine hivyo bado huduma shirikishi zitaendelea kutolewa zikiambatana na huduma bobezi za magonjwa ya moyo”, alisema Mhe. Ummy

Waziri Ummy alisema Wizara inategemea bunge litapitishia mswada wa bima ya afya kwa wote hivyo kuwataka watanzania wajipime kipi wanataka kuwekeza katika vipaumbele vyao kwa kuona muhimu wa afya kwani bila afya huwezi kufanya shughuli yoyote.

“Tukipitisha sheria ya bima ya afya kwa wote hatutaoneana huruma tena katika kupatiwa huduma za afya, wale wasio na uwezo tutawabainisha kwani bima ya afya kwa wote imeainisha huduma za msingi kwa kuzigawa bima za afya ambazo zitamuwezesha mtu kupata huduma katika Zahanati, vituo vya afya, na hospitali za wilaya za serikali na bima za afya nyingine zitakuwa zinatoa huduma za afya hadi hospitali za kanda na rufaa”,

“Lazima watanzania waone umuhimu wa kuwekeza kwenye afya zao kwani ajenda zetu sasa kama wizara ni pamoja na ajenda ya bima ya afya kwa wote na ubora huduma za afya ambazo zinawataka watoa huduma kuhakikisha kuwa mgonjwa anatumia masaa matatu tu anapofika hospitali na kapata huduma aliyokuwa anaitaka”, alisema Mhe. Ummy

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema magonjwa ya moyo yamezidi kuongezeka hivyo kuongeza idadi ya wagonjwa katika Tawi la JKCI makao makuu.

Dkt. Kisenge alisema Tangu kukabidhiwa kwa hospitali ya JKCI Dar Group idadi ya wagonjwa wanaopatiwa huduma katika Hospitali hiyo imeongezeka kutoka wagonjwa 400 kwa siku hadi kufikia wagonjwa 600 kwa siku. 

“Tunawahakikishia wananchi kwamba watapata huduma zetu nzuri kwani madaktari bingwa wa moyo tayari wameshaanza kutoa huduma zetu katika Hospitali hii lakini pia tumeshaleta vifaa tiba vyenye gharama zaidi ya shilingi milioni 500 eneo la huduma za dharura”, alisema Dkt. Kisenge

Akizungumzia kuhusu bima ya afya kwa wote Dkt. Kisenge alisema muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote utakapopitishwa wananchi wajitokeze kwa wingi kukata bima ya afya kwani gharama za kutibu magonjwa ya moyo ni kubwa tofauti na magonjwa mengine.

“Mgonjwa mwenye tatizo la kuziba kwa mshipa wa moyo inamgharimu hadi shilingi milioni 6 kupatiwa matibabu, na mgonjwa anayehitaji kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo humgharimu hadi shilingi milioni 15”, alisema Dkt. Kiseng

Hospitali ya Dar Group ilikuwa Hospitali iliyojengwa kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wafanyakazi wa viwandani na kuendeshwa na watu wa vyama vya wafanyakazi ambapo ilisajiliwa na msajiri wa Hazina Wizara ya Afya kama Taasisi ya umma na kufikai Novemba mwaka 2022 hospitali hiyo ikakabidhiwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya kupanua wigo wa utoaji wa huduma za matibabu ya moyo.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akitembelea Hospitali ya JKCI Dar Group kuangalia utoaji wa huduma na mwelekeo wa Hospitali hiyo baada ya kuikabidhi kuwa chini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tangu mwezi Novemba 2022.


No comments