BARAZA KUU LA UONGOZI CUF TAIFA LAMPONGEZA RAIS SAMIA KUONDOA ZUIO LA MIKUTANO YA HADHARA
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama Cha Wananchi (CUF) limepongeza hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuondoa zuio haramu la Mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa.
Akisoma maadhimio ya kikao hicho jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipimba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ya kikao chake cha Januari 21 hadi 22 mwaka huu.
Alisema Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi kuwa “Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.”
Pia alisema Ibara ya 11(1)(a) ya Sheria ya Vyama vya Siasa inavipa haki Vyama vya Siasa kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima. Rais hana mamlaka ya kuzuia mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa. Tunampongeza Dr Samia kwa kutambua hili na kuacha kuendelea kuivunja Katiba ya nchi na sheria ya Vyama vya Siasa,
Prof lipumba aliongeza kuwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeupongeza Uongozi wa Chama hicho Wilaya ya Ubungo kwa kufanya Mkutano wa Hadhara Januari 7, 2023 katika eneo la Manzese, Wilaya ya Ubungo.
Amebainisha kuwa mkutano huo ulifanyika siku ya nne baada ya kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara ya kisiasa, na CUF kuwa Chama cha kwanza kufanya mkutano wa hadhara.
Aidha amesema Baraza Kuu limewaelekeza wajumbe wote wa Baraza Kuu, viongozi na wanachama wa ngazi mbali mbali kuendelea kufanya mikutano ya hadhara kwenye maeneo yao, kuelezea na kueneza sera za CUF za Haki Sawa na Furaha kwa Wananchi.
Katika hatua nyingine Profesa lipumba alizungumzia ubunge wa Afrika Mashariki, ameeleza kuwa Baraza Kuu limempongeza kwa dhati Wakili Msomi Mashaka Ngole kwa kuchagualiwa kuwa Mbunge wa Afrika Mashariki katika Uchaguzi uliofanyika Septemba 22, 2022.
Alisema Baraza Kuu pia limemuagiza Mashaka Ngole awe Mbunge mahiri wa mfano katika kutetea maslahi ya Watanzania ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumzia taarifa ya kikosi kazi Prof. Lipumba amesema Baraza Kuu limesikitishwa na muda mrefu uliotumiwa na Kikosi kazi kilichoundwa chini ya ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufuatia mkutano baina ya Msajili na Vyama vya Siasa na wadau wengine wa demokrasia, kukamilisha taarifa yake iliyowasilishwa kwa Rais Oktoba 21, 2022.
“Kikosi kazi kimetumia zaidi ya miezi 10 kwa ajili ya zoezi hilo. Kwenye Mkutano uliofanyika tarehe 15-17 Desemba 2021 jijini Dodoma, mambo yote ya msingi yalijadiliwa na kuanishwa. Mwezi mmoja ulitosha kabisa kwa Kikosikazi kidogo kuandaa taarifa ili Serikali iifanyie kazi kabla ya kupitisha bajeti yake ya 2022/23; ili yale yaliyokubaliwa yaanze kutekelezwa,” amebainisha Prof. Lipumba.
Ametaja baadhi ya mambo muhimu yaliyoafikiwa kuwa ni pamoja na kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya itakaozingatia maoni ya wananchi yaliyotolewa kwenye Tume ya Jaji Warioba na Kuanzishwa Tume Huru ya Uchaguzi kama ilivyoanishwa katika Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na kuingizwa ndani ya Katiba Inayopendekezwa.
Mengine ni Tume huru isimamie chaguzi zote zikiwemo za serikali za mitaa, Uchaguzi wa ZEC Zanzibar ufanyike siku moja na Vyama vya siasa vifanye mikutano ya hadhara kwa mujibu wa sheria. Taarifa za mikutano ya hadhara ziwasilishwe kwenye kituo cha polisi kilicho jirani na eneo la mkutano.
Amebainisha mengine ni Vyama vya siasa viwajibike kisheria kuwa na walau theluthi moja ya wajumbe wake katika vikao vya maamuzi kuwa ni wanawake, Sheria ya Jeshi la Polisi ipitiwe upya ili Jeshi la Polisi liheshimu haki za raia na liendeshwe kwa weledi na uwajibikaji, Sheria ya Vyama vya Siasa ya 2019 ipitiwe upya kuirekebisha kwa lengo la kuimarisha demokrasia; naP na mchakato shirikishi wa kuandaa Dira Mpya ya Taifa.
Prof. Lipumba ameongeza kuwa Baraza Kuu limebaini kuwa Taarifa ya Kikosi kazi haikuweka baadhi ya mambo muhimu yaliyoafikiwa katika Mkutano wa Dodoma.
Ameeleza mambo hayo kuwa ni pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi; Tume Huru ya Uchaguzi iwe na Watendaji wake yenyewe; Sheria ya Polisi ipitiwe upya ili Jeshi la Polisi liheshimu haki za za raia na liendeshwe kwa weledi na uwajibikaji; Sheria ya Vyama vya Siasa irekebishwe kuimarisha demokrasia; na pawepo na mchakato shirikishi wa kuandaa dira mpya ya taifa.
Kwamba Baraza Kuu linaishauri Serikali kuweka kalenda ya utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosikazi hususan kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Pia Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linaitaka Serikali kuweka kipaumbele katika mchakato wa kupata Tume Huru ya Uchaguzi, kwa sababu ya muda mfupi uliobaki kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji 2024; na Uchaguzi Mkuu, 2025.
Kwamba umuhimu wa Tume Huru umejidhihirisha kwenye Chaguzi za marudio kwenye majimbo na Kata. Chaguzi ndogo zilizofanyika katika jimbo la Amani, Zanzibar na kata mbalimbali nchini zimeonyesha wazi kwamba bado wasimamizi wa Uchaguzi wanaendeleza kile kilichofanyika kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020.
“Ili kujenga demokrasia na kuepuka vurugu za kisiasa ni muhimu sana kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi yenye Watendaji wake muhimu, mapema iwezekanavyo, ili Tume hiyo iweze kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024; na Uchaguzi Mkuu wa 2025,” amesema.
Aidha amesema Baraza Kuu limestushwa na kauli ya Dr. Ali Uki, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais wa Zanzibar alipokuwa anawasilisha Taarifa ya Kikosikazi hicho kwa Rais Hussein Mwinyi, kwamba moja ya Mapendekezo ya Kikosikazi hicho ni kuendelea na kuwa na Uchaguzi unaoruhusu kura ya mapema, yaani kwa uchaguzi wa Zanzibar.
“Pendekezo hili halina sababu za msingi zenye mashiko hasa ukizingatia kuwa Wazanzibari wanashiriki Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano unaofanyika siku moja,”.
Kwamba Baraza Kuu linamtaka Rais wa Zanzibar kulitupilia mbali pendekezo hili la Kikosikazi cha Dr. Uki, na badala yake Uchaguzi wa Zanzibar uwe wa siku moja tu kwa wapiga kura wote, kama ilivyopendekezwa na Wadau wa Demokrasia katika Mkutano wa Dodoma wa Desemba 2021.
No comments