Breaking News

VITENDO VYA DHALILISHAJI NA UKATILI WA NGONO VYAONGEZEKA

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema kuwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kingono katika Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam vimeongezeka.

Akizungumza jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Wakili Anna Henga wakati akitambulisha mradi wa majaribio unaolenga kuzuia na kukabiliana na udhalilishaji na unyanyasaji wa kingono.

"Kwamujibu wa utafiti uliofanyika na Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mwaka 2019/2021 ilibainika kuwa Vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kingono katika Wilaya ya Kinondoni vimeongeka ambapo tulibaini kuna Matukio takribani 57,626 na kati ya hayo mengi yalikuwa udhalilishaji na ukatili wa kijinsia hasa udhalilishaji wa kingono," alisema Henga.

Henga alibainisha kwamba utafiti mwingine wa LHRC pia umenonesha kwamba Makundi Maalum, ambayo yanajumuisha watoto, watu wenye ulemavu, na wanawake, yaliathiriwa zaidi na janga la ugonjwa wa Korona mwaka 2020.

Alisema kwa upande wa watoto, janga hili liliilazimu Serikali kufunga shule na watoto kurudi nyumbani kwa takribani miezi mitatu, na katika kipindi hiki ambacho watoto walikuwa nyumbani kuliripotiwa kuongezeka kwa matukio ya ukatili dhidi yao, hasa ukatili wa kingono na mimba za utotoni.

Mkurugenzi huyo alisema kutoka mwaka 2018 hadi 2020, LHRC imekusanya zaidi ya matukio 2,991 ya mimba za utotoni yaliripotiwa katika mikoa mbalimbali.

"Kwa mwaka 2020, LHRC ilikusanya matukio 448 ya mimba za utotoni, ambayo yaliripotiwa katika mikoa 15 ya Tanzania Bara katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Disemba, matukio mengi yakihusisha wasichana wenye umri wa miaka 13 hadi 17. Wasichana waliopata mimba walilazimika kuacha shule, hivyo kupoteza haki yao ya elimu, sambamba na kufanyiwa vitendo vya kibaguzi," aliongeza.

Aliutaka umma utambue kuwa vitendo au masuala ya unyanyasaji na udhalilishaji wa kingono ni kosa la jinai, kwa Mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai sura ya 16 kuanzia kifungu cha 130 na kuendelea inaeleza na kutaja adhabu ya makosa hayo.

"Hivyo tunakila sababu ya kutetea na kuvipinga vikali vitendo hivi katika jamii zetu," alisema Henga.

Akizungumzia mradi huo Henga alieleza kwamba LHRC imeingia makubaliano na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kuutekeleza wenye lengo la kujenga uwezo na kuhamasisha wadau mbalimbali ili kuweza kuzuia na kukabiliana na changamoto za matukio ya udhalilishaji wa kingono kwa makundi mbalimbali na kufanya tathmini ya jinsi ya kuandaa program za udhalilishaji na unyanyasaji wa kingono zenye tija na ufanisi.

Alisema mradi huu unatekelezwa katika Hospitali ya Mwananyamala ambayo ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dar es Salaam na jamii inayoizunguka zikiwemo Kata za Mwananyamala na Makumbusho.

"Mradi huu ambao ni wa majaribio kwa kipindi cha miezi takribani mitatu (3), unatekelezwa kwa pamoja na wadau wengine wakiwemo Madiwani, Wenyeviti na Watendaji wa Serikali za Kata na Mitaa Katika Eneo la Mradi, Dawati la Polisi la Jinsia na Watoto, Watendaji wa Kata na Mitaa, Maafisa wa Elimu.

"Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii Ngazi ya Mkoa, Manispaa na Kata; Wanafunzi na Waalimu wa Shule za Sekondari na Msingi Katika Eneo la Mradi, Klabu za Michezo, Madereva wa Bodaboda; Waandishi wa Habari, Asasi za Kiraia na wadau wengine wenye kunia mamoja na malengo ya mradi,".

Alisema mradi huo utatekelezwa katika awamu kuu sita.

No comments