Breaking News

BI MAIMUNA SAID AREJESHA FOMU YA KUWANIA KUTEULIWA NA CHAMA CHA ADC KUGOMBEA NAFASI YA SPIKA WA BUNGE

Kada wa Chama Cha Alliance For Democratic Change( ADC) Bi Maimuna Saidi leo 16 January amerejesha fomu makao makuu ya Chama jijini Dar es salaam kwa ajili ya Kuomba Kuteuliwa na chama chake  kugombea Nafasi ya Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiongea na Waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi fomu hiyo kwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu Bara, Bi. Maimuna amesema kwa dhati ameamua kugombea nafasi hiyo na endapo Chama kitamteua na wabunge kumchagua kuwa spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jambo la kwanza nitaanza kwa kuhakikisha naunganisha mihimili ya serikali Mahakama, Bunge na Serikali ili ifanye kazi kwa ushirikiano.

"Kwa mujibu wa katiba ni haki yangu kikatiba kugombea nafasi hii ya Uspika, nikipitishwa na chama na kisha wabunge nao kunichagua cha kwanza nitahakikisha Bunge linakua na ushirikiano na mihimili mingine ili ifanye kazi kwa pamoja haki na sawa katika kusimamia, kukosoa na kushauri Serikali" Alisema Bi. Maimuna.
Mapema akizungumza mara baada ya kupokea fomu Kaimu Naibu Katibu Mkuu Bara, Bw. Doni Mnyamani alisema hadi sasa bado mwachama mmoja wa chama hicho aliyejitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kikao cha kamati tendaji ya Chama hicho inatarajiwa kuketi Januari 20 kwa ajili yakupitisha jina la mgombea mmoja ili lipelekwe Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

"Leo Bi Maimuna Saidi amerudisha fomu ambayo alichukua jumapili ya tarehe 16 Kuomba kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya aliyekua Spika wa Bunge hilo Job Ndugai kujiuzulu, mpaka sasa tuna mtu mmoja tu aliejitokeza kuchukua fomu" Alisema Bw.Mnyamani

Aidha bw. Mnyamani aliongeza kuwa tarehe 20 mwezi huu kamati kuu tendaji ya chama itakutana kupitisha jina la mgombea atakaye kiwakilisha chama na jina lake kulipeleka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya taratibu zingine hivyo kutoa wito kwa wanachama kuendelea kujitokeza kuchukua fomu.

No comments