Watanzania Changamkieni Fursa Zinazojitokeza Kufatia Kukinga na “AMCOMET”
Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Ndg. Amour Hamil Bakari, amewaasa Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazojitokeza baada ya Tanzania kujiunga na “AMCOMET”.
Aliyasema hayo alipokuwa akifungua rasmi kikao cha kupata maoni ya wadau kuhusiana na mapendekezo ya kusaini Katiba ya Baraza la Mawaziri wenye dhamana ya Hali ya Hewa katika Bara la Afrika, yaani “African Ministerial Conference on Meteorology (AMCOMET)”
“Naomba nitumie fursa hii kupitia ufunguzi wa kikao hiki cha kupata maoni ya mapendekezo ya kusaini katiba ya Baraza la Mawaziri wenye dhamana ya Hali ya Hewa - Barani Afrika, kuwaasa Watanzania kutumia fursa mbalimbali zikiwemo za ajira zitakazojitokeza baada ya kujiunga na “AMCOMET”.” alisema Katibu Mkuu Amour Hamil Bakari.
Aidha, Ndg. Bakari aliongezea kuwa uchumi wa nchi yetu pamoja na nchi zingine zinazotuzunguka unategemea zaidi sekta za kiuchumi na kijamii ambazo hutegemea na kuathiriwa sana na hali ya hewa, hususan kwa kuzingatia kuwa hali ya hewa haitambui mipaka ya kijiografia, hivyo nchi zinazofanana katika mifumo ya hali ya hewa zimekuwa na programu za pamoja za kikanda na kimataifa ili kupata suluhisho la kupunguza athari za majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Muwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) (SMT) Ndg. Biseko Paul Chiganga, alisisitiza kuendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala ya muungano baina ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (SMT) pamoja na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (SMZ), ukilenga kuweka uelewa wa pamoja na baadae kutatua changamoto mbalimbali baina ya sekta za hali ya hewa na usafiri wa anga na sekta nyingine mtambuka.
Aidha, Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Ndg. Mohammed Ngwali, alimshukuru mgeni rasmi kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kikao hicho muhimu cha kupokea maoni ya wadau kitakachoiwezesha Tanzania kupiga hatua zaidi katika mchakato wa kusaini katiba ya “AMCOMET”
No comments