Breaking News

TMA Yatoa Mafunzo Kwa Watumishi wa Kada ya Huduma Saidizi Mchanganyiko

Pwani; 
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mafunzo ya kujenga uelewa wa huduma za hali ya hewa kilimo kwa watumishi wa kada ya huduma saidizi ili kuongeza usambazaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika shughuli za kilimo. Mafunzo hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wakunga na Manesi, Kibaha, Pwani, tarehe 22-23 Oktoba, 2021.

Akizungumza wakati akifungua Warsha ya Watumishi wa Kada ya Huduma Saidizi mgeni rasmi, ambaye ni Mkurugenzi wa Tehama na Huduma za Ufundi TMA Dkt. Pascal Waniha alisema mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wa kuboresha upatikanaji, uelewa na matumizi ya taarifa za hali ya hewa ili kusaidia katika kufanya maamuzi sahihi katika shughuli mbalimbali za kilimo.
“Katika kufanikisha adhima hii, Mamlaka imeona ni vyema kutoa mafunzo kwa watumishi wa kada ya huduma saidizi kwani kutokana na shughuli zenu za kila siku licha ya kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, shughuli zenu za nje ya kazi kama vile bustani na kilimo zimekuwa zikiathiriwa kutokana na hali ya hewa hivyo kupitia warsha hii mtaweza kuelewa huduma mbalimbali zitolewazo na TMA na mtakuwa na jukumu la kusaidia kuzitafsiri, kuzitumia na kuzisambaza taarifa hizi kwa wadau ili waweze kukabiliana na changamoto zinazotokana na athari ya mabadiliko ya hali ya hewa”. Alizungumza Dkt. Waniha.
Awali, wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa TMA alimshukuru Mkurugenzi Mkuu wa TMA kwa warsha hii kwani imekuwa sehemu ya historia na kuwahimiza watumishi kujifunza zaidi na zaidi.

“Kila siku ni fursa, kama tumepewa fursa ya kuwa sehemu ya historia basi sisi wenyewe tunatakiwa tuwe historia kwa namna tunavyoishi na kwa namna tunavyofanya kazi”. Alisema Dkt. Chang’a.
Kwa upande wa watumishi, waliishukuru TMA kwa kuandaa na kuwawezesha kushiriki katika warsha hii ya kujenga uelewa wa huduma za hali ya hewa kilimo ambayo haijawahi kutokea na kuomba mafunzo haya kuwa endelevu.



No comments