Breaking News

MAJALIWA: Anzeni Kutoa Huduma Kupitoa Vituo Vya Huduma Pamoja

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi za Serikali ambazo haziajaanza kutoa huduma kupitia vituo vya huduma pamoja vya Shirika la Posta Tanzania zijipange na zihakikishe zinaanza kutoa huduma katika vituo hivyo ndani ya mwaka huu wa fedha.
 
Amezitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni Tume ya Ajira, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Septemba 6, 2021) wakati akizindia Vituo vya Huduma Pamoja vya Shirika la Posta Tanzania kwenye viwanja vya Posta Makao Makuu jijini Dar es Salaam. Huduma Pamoja ni vituo vitakavyotoa huduma zote za Serikali katika eneo moja kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Taasisi ambazo tayari zimeanza kutoa huduma kupitia vituo hivyo ni RITA, UHAMIAJI, NIDA, BRELA, TRA, PSSSF, NSSF na Halmashauri za Majiji, hivyo Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kupata huduma ambapo kwa sasa huduma hizo zinatolewa katika vituo vilivyopo kwenye ofisi za Posta za Dar es Salaam na Dodoma.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa sh. bilioni 3.9 kwa ajili ya maboresho ya shirika hilo kwa mfumo wa kidijitali.

“Tumepokea fedha hizo na bado tutapokea bilioni 3.9 fedha hizi hazina posho wala semina, zote zinakwenda kuboresha mfumo wa shirika hilo na kuwa wa kidijitali.”
Awali, Kaimu Posta Masta Mkuu, Macrice Mbodo alisema mradi huo wa vituo vya huduma pamoja ni sehemu ya miradi ya Tanzania ya kidijitali ambapo katika mradi huo Serikali imetenga jumla ya Dola za Marekani 21,500,000 sawa na shilingi 49,536,000,000.

Alisema utekelezaji wa mradi huo umegawanyika katika awamu kuu tatu ambapo awamu ya kwanza itahusisha vituo 10 navyo ni Dar es Salaam (Posta Kuu-GPO), Dodoma (Posta Kuu), Arusha (Posta Kuu), Mbeya (Posta Kuu), Morogoro (Posta Kuu), Mwanza (Posta Kuu), Tanga (Posta Kuu), Kigoma (Posta Kuu), Mjini Magharib (Posta Kijangwani) na Kaskazini Pemba (Chake Chake).

No comments