Breaking News

Dkt. JINGU: Tanzania Bado Kuna Changamoto ya Watoto wa Mtaani

Inaelezwa kuwa Tanzania inakabiliwa  na tatizo la kuwa na watoto wa mitaani na kwa takwimu zilizopo ni kwamba inakadiriwa kuwa na  idadi ya watoto 35,919 wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika majiji na miji mbalimbali licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali pamoja na Wadau kutokomeza tatizo hilo.

Hayo yamebainika wakati wa kikao kazi cha Makatibu Tawala Mikoa, Makamanda wa Polisi Mikoa na Wadau wanaohusika na masuala ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kilichofanyika leo Jijini Dodoma.

Akifungua kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema tafiti mbalimbali zimefanyika ili kubaini hali halisi ya watoto hawa mathalani “Head Count Survery” ya mwaka 2017 katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya, Iringa na Dar es salaam ilibaini jumla ya watoto 6,393 ambao walikuwa wanaishi na kufanya kazi mtaani.

Dkt. Jingu amesema kuwa kundi hili ni kubwa na linapokuwepo katika jamii yoyote ni changamoto kwa Ustawi na Maendeleo ya Jamii husika kwani athari mojawapo ni watoto hao kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu.

“Kundi hili ambalo badala ya kwenda shule wanakaa Mitaani wakijilea au kulelewa na watu wasiokuwa na maadili, katika mazingira yasiyo salama na wanafanyiwa ukatili hivyo kujikuta wakijiingiza kwenye uhalifu, tatizo hili likiendelea tunatengeneza tatizo la kijamii kwa sababu kuna watu watakuwa hawajapata malezi yanayostahili” amesema Dkt. Jingu.

Na Mwandishi WAMJW, Dodoma

No comments