Breaking News

DC JOKATE: Tushikiane Kuipamba Temeke

Mkuu wa wilaya ya Temeke Mheshimiwa Jokate Urban Mwegelo leo Septemba 20,2021 amefanya kikao na viongozi wa machinga wilaya ya Temeke, watendaji wa mitaa, kata na kamati ya ulinzi na usalama kuangazia suala zima la uhamishwaji wa wafanyabiashara ndogo ndogo (Wamachinga) kwenda kwenye maeneo rasmi. 

Katika kikao hicho Mhe. Jokate aliwakumbusha wafanyabiashara hao nia njema ya serikali juu ya mpango huo. 

"Ni imani yangu hatuwezi kukosana, hatuwezi kutengana ndio maana tumekutana tuzungumze pande zote kwa uwazi, kama Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alivyotoa maelekezo tupange mji wetu kuweka ustaarabu, naamini hatutoshindwa kuelewana huku tukitambua nia njema ya serikali ni kuwasaidia wafanyabiashara siku zote, kupitia kikao hiki tutasaidiana kufikia muafaka mzuri ili tuipendezeshe Temeke yetu" alisema DC Jokate. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Machinga Temeke ndugu John Packsence  ameiomba serikali kuzingatia wingi wa Machinga, maeneo watakayo pelekwa na namna bora ya kwenda na mchakato huo. 

Aidha afisa biashara manispaa ya Temeke ndg. Mohammed Tajiri alisema anatarajia zoezi hilo litaenda vizuri kutokana na ushirikiano uliopo baina ya kamati iliyoundwa kushughulika na zoezi hilo na Wamachinga na viongozi wa Serikali. 

Kikao hiki ni mwazo wa utekelezaji wa agizo la Waziri mkuu Kassim Majaliwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mhe.  Amos Makalla kupanga mji kwa kuondoa wafanyabiashara wadogo wadogo katika maeneo yasiyo rasmi.

No comments