Darasa la Saba Waanza Mtihani Leo
JUMLA ya wanafunzi 1,132,143 wa darasa la saba waliosajiliwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), leo na kesho watafanya mitihani ya taifa ya kuhitimu elimu ya msingi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mitihani hiyo Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema maandalizi yamekamilika na mitihani imeshazambazwa kwenye vituo.
“Watahiniwa 1,132,143 wamesajiliwa kufanya mtihani mwaka 2021, kati ya hao 1,079,943 sawa na asilimia 95.39 watafanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na 52,200 sawa na asilimia 4.61 watafanya mtihani huo kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia,” alisema Dk Msonde.
Alisema katika mtihani huo idadi ya masomo itakayotahiniwa imeongezeka kutoka masomo matano ya mwaka jana na kuwa sita na hiyo ni kwa mujibu wa mtaala mpya ambao ulianza kutumika wanafunzi hao wakiwa darasa la kwanza.
Somo lililoongezeka linaitwa uraia na maadili ikiwa ni sehemu ya maboresho ya masomo na kwamba masomo mawili yameboreshwa maudhui yake ambayo ni sayansi ambalo sasa linaitwa sayansi na teknolojia na maarifa ambalo sasa linaitwa maarifa ya jamii na stadi za kazi.
No comments